Mbeya. Hospital ya Rufaa Kanda ya Mbeya (MZRH) imepokea kitanda cha kisasa cha upasuaji chenye thamani ya Sh37 milioni ambacho kinatumia mifumo ya kidigitali na nishati ya umeme.
Kitanda hicho kina vifaa vya kisasa ambavyo vitawawezesha madaktari wawili au mmoja kufanya oparesheni ambayo ingefanywa na madaktari sita mpaka saba.
Umoja wa wanawake watumishi wa hospitali hiyo wametoa kitanda hicho baada ya kujichanga posho, mishahara na sehemu ya vipato vyao vya kiuchumi kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utoaji huduma za kibingwa.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa kitanda hicho leo Aprili 19, 2024, mkuu wa idara ya upasuaji, Dk Lazaro Mboma amesema mifumo ya kitanda hicho ni tofauti na vitanda vingine kwa sababu kinatumia nishati ya umeme na teknolojia za kidigital wakati wa kuandaa kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa.
“Kitanda cha kipekee tofauti na tulivyovizoea kwani kinatumia zaidi teknolojia za kidigitali wakati wa kutoa huduma za upasuaji kwa kutumia kifaa kwa mbali (remote control), jambo ambalo litasaidia kutoa huduma za kibingwa kwa ufanisi mkubwa,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa Kanda Dk, Godlove Mbwanji amesema kitendo kilichofanywa na umoja wa wanawake ni sadaka na kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita katika kuboresha huduma za afya nchini.
Mkuu wa kitengo cha mifupa, Dk John Mbanga amesema wanakwenda kuongeza weledi mkubwa na ufanisi kwa madaktari bingwa kutokana na uwezo mkubwa wa vifaa vilivyotolewa kupitia kitanda hicho.
Mwenyekiti wa umoja wa wanawake MZRH, Stella Nkwama amesema wameona ni vyema kuchangia huduma za afya kwa kujichanga posho, mishahara na sehemu ya faida katika biashara zao kununua kitanda hicho cha kisasa chenye thamani ya zaidi ya Sh37 milioni.
“Siku ya wanawake tuliitumia kugusa jamii nyingine, lakini leo tumeona turejee nyumbani kuchangia kitanda cha kisasa cha upasuaji chenye thamani ya Sh37 milioni ili kuboreshwa huduma za kibingwa katika kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kwenye uwekezaji wa sekta ya afya,” amesema.
Naye katibu wa umoja huo ambaye pia ni Mkurugenzi wa rasilimali watu, Miriam Msalale amesema wamelazimika kujichanga sehemu ya posho, mishahara na kipato kitokanacho na shughuli zao za kiuchumi kurejesha kwa jamii kuchangia huduma za afya.
Mkazi wa Njombe, Daniel Naftari anayepata tiba ya mifupa, amesema awali walikuwa wakienda Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), kupata matibabu kutokana na hospitali ya Kanda kutokuwa na madaktari bingwa lakini sasa imekuwa kimbilio.