Tanga. Madereva wa mabasi madogo yanayofanya safari zake kati ya Tanga mjini na Horohoro Wilaya ya Mkinga waliogoma jana Mei 2, 2024 kusafirisha abiria, leo Ijumaa Mei 3, 2024 wameendelea na kazi kwa makubaliano ya kutoza Sh3, 500 hadi Jumatatu, pande tatu zitakapokaa kujadiliana.
Madereva hao walikuwa wanapinga uamuzi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) kutaka abiria watozwe Sh3,200 badala ya Sh3,500.
Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa kituo cha mabasi cha Mwembe Mawazo, Madawa Salimu amesema wamekubaliana na Latra pamoja na Jeshi la Polisi wanaendelee na safari zao kwa kutoza Sh3, 500 hadi Jumatatu Mei 6 watakapokaa na kujadiliana upya.
Amesema upande wao (madereva) watakutana kesho Jumamosi Mei 4, 2024 kujadili na kupanga mikakati yao kabla ya kikao cha Jumatatu.
“Tumeruhusiwa na Serikali – Latra na Polisi – tuendelee na safari kwa nauli ya Sh3,500 hadi Jumatatu tutakapokutana kwenye kikao,” amesema mwenyekiti huyo.
Ofisa Mfawidhi wa Latra mkoani Tanga, Shedrack Malale amethibitisha suala hilo.
“Tumeruhusu waendelee kutoa huduma kwa nauli wanayoitaka wao ya Sh3,500 ili wananchi waendelee kupata huduma, lakini bado tunatafuta mwafaka wa hilo na Jumatatu ndiyo itajulikana,” amesema Malale.
Abiria Sabrina Michael, mkazi wa Mkinga aliyezungumza na Mwananchi, amesema ni vizuri Serikali na mamlaka nyingine kama kuna jambo lenye masilahi kwa wananchi, litatuliwe mapema kabla halijaleta madhara.
“Barabara ya kwenda Horohoro ni moja na eneo hilo lina watu wengi sana, mgomo kama huu unatuathiri mno, kumbuka barabara hii inatumiwa pia na watu wanaovuka mpaka wa Tanzania wanaosafiri kwa mabasi, kukaa siku nzima bila kuwa na usafiri wa uhakika ni shida,” amesema Michael.
Naye Mohammed Ally mkazi wa Horohoro amesema haoni sababu ya madereva kung’ang’ania kupandisha nauli wakati tayari Serikali imeshaweka viwango vyake, huko ni kuwanyanyasa wananchi.
“Siku zote matajiri wanapenda wao wapate zaidi, hawajui na sisi tunaumia, hii nauli ya Sh3, 200 inatosha kabisa na sababu wanazotoa binafsi hainiingii akilini, hiyo Jumatatu wakikaa mimi napendekeza Serikali isiwasikilize ibaki na msimamo wake ule ule,” amesema Ally.