MAMA LISHE WATOA WITO KWA WADAU

Wafanyabiashara wa chakula maarufu kama ‘Mama Lishe’ wametoa wito kwa wadau wa maendeleo kushirikiana nao katika kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili biashara zao, hususan ukosefu wa vifaa vya kisasa na mitaji ya kuimarisha biashara.

 Wafanyabiashara hao walitoa wito huo kupitia ‘Coca-Cola Food Fest’, tamasha la chakula lililoandaliwa na Kampuni ya Coca-Cola, wakibainisha kuwa matamasha kama hayo yanasaidia sana kuongeza ujuzi na ufanisi katika biashara zao.

Akizungumza katika tamasha hilo, ‘Mama Lishe’ Veronica Athanas alisema, “Matamasha kama haya yanatupa fursa ya kipekee kujifunza na kuboresha uendeshaji wa biashara zetu, jambo ambalo linatusaidia sana kuongeza kipato.” 

Mwenzake Asha Mohammed aliongeza, “Kupitia tamasha hili, tumepata fursa ya kujifunza mbinu za kisasa za kuboresha biashara zetu na tunawaomba wadau wengine zaidi wajitokeze kusaidia juhudi hizi.”

Wafanyabiashara hao waliishukuru Kampuni ya Coca-Cola kwa kuandaa tamasha hilo, wakisema limewapa uelewa mpya wa mbinu za kuendesha biashara, huku wakisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa sekta binafsi na Serikali katika kuwasaidia kupata vifaa vya kisasa na mitaji ili kuboresha zaidi biashara zao.

Walihitimisha kwa kutoa wito kwa wadau wa sekta mbalimbali kuwekeza zaidi katika kusaidia wafanyabiashara wadogo kama ‘Mama Lishe’, kwa kuwa msaada huo si tu utaboresha biashara zao, bali pia utaimarisha hali za kiuchumi za familia na jamii kwa ujumla.





Related Posts