NSSF KUFIKISHA HUDUMA KWA WATEJA KIDIJITALI ZAIDI

Naye, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Bw. Omary Mziya, amesema wanaendelea kuboresha huduma za wateja siku hadi siku kwa kuwa umuhimu wa wateja ni mkubwa na ndio sababu za kuwepo kwa NSSF.

Amesema wanachama wachangiaji wa NSSF wameongezeka kutoka 1,189,000 mwezi Juni 2023 na kufikia 1,342,654 mwezi Juni 2024. Idadi ya wanufaika wa Pensheni nao wameongezeka ambapo mpaka kufikia mwezi Juni 2024 wamefikia wastaafu 31,914.

Bw. Mziya amesema wanufaika wa mafao mengine wakiwemo wa Matibabu wamefikia 207,229 mpaka kufikia Juni 2024 na kuwa idadi ya waajiri imeongezeka na kufikia 41,616.

Amesema wanufaika wa Mafao ya Uzazi mpaka kufikia Juni 2024 walikuwa 10,809, wanufaika wa Mafao ya Kupoteza Ajira mpaka kufikia Juni 2024 walikuwa ni 109,286. “Hivyo utaona idadi ya wateja wetu imekuwa ikiongezeka siku hadi siku na sisi kipaumbele chetu ni kuendelea kutoa huduma bora na kuongeza idadi ya wanachama wengi zaidi,” amesema Bw. Mziya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Ekwabi Mujungu ameahidi kuwa wafanyakazi wataendelea kusikiliza wateja, kutoa huduma za kipekee, kuwasiliana kwa uwazi, kujitolea kwa wateja kwa maana ya kuvaa viatu vyao, kujifunza na kuboresha huduma kila siku, lengo ni kupunguza malalamiko.

Naye Robert Kadege, Meneja wa Huduma kwa Wateja, amesema Wiki ya Huduma kwa Wateja ilianza kuadhimishwa rasmi mwaka 1987 kwa lengo la kutambua umuhimu wa huduma bora kwa wateja pamoja na wafanyakazi wanaotoa huduma bora kwa wanachama.

Amesema NSSF inatumia wiki hii kwa ajili ya kukumbushana umuhimu wa huduma bora kwa wateja na kuwashukuru kwa namna ambavyo wanaunga mkono juhudi mbalimbali za NSSF ambapo kwa sasa imejikita katika kuboresha huduma zake kupitia mifumo ya kidijitali.

Awali, Meneja wa NSSF Mkoa wa Mbeya, Bw. Deus Jandwa amewahakikishia wateja kuwa wanaendelea kutoa huduma bora za hifadhi ya jamii, kutatua kero mbalimbali pamoja na kufikisha elimu ya hifadhi kwa sekta binafsi na sekta isiyo rasmi.

Related Posts