Dar es Salaam. Taasisi Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imesema inafuatilia taarifa zozote za rushwa katika uchaguzi, zikiwemo zilizotolewa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu kuwa kuna fedha zimemwagwa kwenye uchaguzi wa ndani wa chama hicho.
Lissu alitoa madai hayo jana Mei 2, 2024 alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara mjini Iringa, akihoji fedha hizo zimetoka kwa nani?
“Leo kwenye uchaguzi kuna hela ya ajabu, ninyi mnafikiri hiyo hela ni ya wapi? Mnafikiri hiyo hela ni ya nani? Mnafikiri hiyo hela itatuacha salama? Ukitaka kujua kwamba hatuko salama, fuatilia mitandaoni,” alisema.
Akizungumza na Mwananchi leo Mei 3, 2024, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Salum Hamduni amesema taasisi yake inafuatilia taarifa hizo na si lazima zipelekwe kiofisi.
“Taarifa kwa kawaida sisi tunapokea kutoka kwenye chanzo chochote kile, sio lazima mtu afike kwenye ofisi, kwa hiyo ama taarifa imetoka hadharani inaangukia kwenye mamlaka ya kisheria ya Takukuru, inafanyia kazi,” amesema.
Alipoulizwa kama wameshaanza kuzifuatilia taarifa hizo na kama watamwita Lissu kumhoji amesema: “Hilo ni suala la kiuchunguzi na la kiofisi, tukilazimika na tukaona kwamba kuna ulazima wa (Lissu) kuitwa ataitwa.”
Mwananchi imemtafuta Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kuhusu madai hayo, lakini alimwambia mwandishi atampigia baadaye, na hadi taarifa hii inachapishwa hakuwa amempigia.
Lissu ametoa madai hayo wakati ambao Kanda ya Nyasa inakabiliwa na ushindani mkali kati ya Mbunge wa zamani wa Iringa, Peter Msigwa na mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Sugu), ambapo kwa mara ya kwanza wafuasi wa kila mgombea wameandamana kwenda kuwachukulia fomu kwa nyakati tofauti.
Leo Msigwa alipoulizwa kuhusu kauli ya Lissu, amesema ameipokea kama kauli ya kiongozi wake wa juu.
“Lissu ni Makamu Mwenyekiti wa chama, ni kiongozi mkubwa kwenye chama chetu, kwa hiyo akiona jambo labda baya au harufu mbaya, analizungumza kama kiongozi wa chama.
Amesema, kama Mwalimu (Julius) Nyerere alivyokemea nyufa za Taifa akitaja udini, Uzanzibari na rushwa.
“Nadhani na Lissu amefanya kama kiongozi, kwamba kuna watu wanatumia hela chafu, kwa hiyo ni wakeup call (wito) kwa chama chetu kama kuna mtu anafanya hayo mambo ajitathmini ili tusiruhusu rushwa ndani ya chama chetu,” amesema.
Kuhusu wafuasi wake kufanya maandamano wakati wa kumchukulia fomu na kama shamrashamra hizo zinaakisi kauli ya Lissu, Msigwa amekanusha.
“Hiyo sio sawa kwa sababu watu wanakua, chama kilivyokuwa miaka 15 iliyopita na kilivyo sasa ni vitu viwili tofauti, watu wanaotaka kugombea kwa sasa ni wengi.
“Zamani chama hiki alikuwa anaweza kuwa mtu mmoja tu anapewa fomu wagombea ni wa kutafuta, kwa hiyo lazima taratibu na hamasa itaongezeka, na hiyo itatoa changamoto kama kuna mambo mengine yanakiukwa, itabidi zitengenezwe kanuni.
“Kama kanuni haikatai, sioni tatizo kuwa na hekaheka za kuchukua fomu. Sioni kama Lissu ameweka allegation (tuhuma) hapo, kwa sababu hajamtaja mtu, amerusha jiwe gizani kama kuna mtu jiwe limemgonga, aache
“Lissu ameonya kama kiongozi, kwamba hizi hela naziona, na mimi naunga mono kwamba ni hatari kwa chama chetu,” amesema Msiwgwa.
Amegusia pia kauli ya Lissu kwamba kuna watu waliokuwa wakizuia asiende katika kanda hiyo kwa madai kwamba alikuwa anakwenda kumpigia kampeni.
“Aliwaambia mnanizuiaje nisiende kwenye kanda, hata Kanda ya Victoria kulikuwa na uchaguzi bado mikutano imefanyika na mwenyekiti alikuwepo, Serengeti kuna uchaguzi na bado mwenyekiti ameenda, kwa hiyo kusema yeye asije kwa sababu kuna uchaguzi ilikuwa ni hoja ya kipuuzi tu ya watu ambao hawajui kinachoendelea ndani ya chama,” amesema.
Sugu alipotafutwa kuelezea kwa upande wake simu imeita bila kupokewa na jitihada za kumtafuta zinaendelea.
Hivi karibuni, akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu, Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba alisema kumekuwa na harufu ya rushwa kwenye chaguzi za vyama.
“Nyingi zinakuwa ni chaguzi za fedha, rushwa na upendeleo, wananchi wanaona kwa kuwa mnateua watu watakaokuja kuwawakilisha, kuanzia huko mnafanya kwa masilahi yenu na sio ya wananchi, hili nalo ni tatizo,” alisema.
Alisema vyama vya kisiasa ni vyombo tu, vipo kwa ajili ya wananchi, wanapofanya tofauti wananchi wanaona, hata chaguzi zao za ndani, wananchi wanaziona na kuona yanayotendeka.