SERIKALI imetoa maagizo tisa kwa watendaji wakuu wa taasisi, mashirika ya umma na wakala wa serikali, kwa lengo la kuongeza ufanisi katika maeneo yao ya kazi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Pwani … (endelea).
Maagizo hayo yalitolewa wilayani Kibaha, mkoani Pwani jana Jumatatu tarehe 07 Oktoba 2024; na Katibu Mkuu katika Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dk. Tausi Kida, kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Moses Kusiluka, wakati wa hafla ya ufunguzi wa mafunzo elekezi kwa watendaji wakuu wapya 111, wa taasisi za umma.
Dk. Kida amewaelekeza kufanya usimamizi madhubuti wa taasisi ili kuwezesha utekelezaji mzuri wa majukumu, kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya serikali na kuendelea kujifunza kwa nia ya kujenga uwezo wa taasisi za umma.
Mengine ni usimamizi madhubuti wa rasilimali watu, fedha pamoja na mali nyingine za serikali, zilizowekezwa katika taasisi.
Katibu Mkuu huyo, amewaelekeza kujenga uhusiano wa kiutendaji wenye afya baina yao na watumishi wanaowasimamia, bodi za wakurugenzi, wizara mama pamoja na wadau wengine.
Amewataka pia kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kubuni vyanzo vipya vya mapato, matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHEMA), mifumo ya utoaji huduma na kujenga maadili mema mahala pa kazi ili kuwezesha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Dk. Kida aliwakumbusha watendaji hao kuwa taasisi na mashirika wanayoyaongoza ni mali ya umma, hivyo umma unatarajia kuona matokeo chanya na yenye maslahi kwao.
“Lazima tuweke mbele maslahi mapana ya Taifa katika kuziongoza taasisi ili nchi ifaidike na uwepo wa taasisi hizi,” alisisitiza.
Dk. Kida amesema lengo la mafunzo kwa watendaji walioteuliwa ni kuwapa ujuzi ili wajue majukumu yanayowakabili kwenye nafasi walizopewa.
Alimpongeza Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, kwa mageuzi yanayoendelea katika utendaji kazi wa taasisi za umma.
“Mageuzi haya kwenye taasisi na mashirika ya umma ni kielelezo tosha cha uongozi imara chini ya Ofisi yako. Natoa wito kuendeleza jitihada hizo ili tuongeze ufanisi,” amesema Dk. Kida.
Kwa upande wake, Mchechu amesema kama watendaji wakuu wakitekeleza ujuzi na mbinu watakazopata katika mafunzo, wataweza kusimamia taasisi zao na kuziendesha kwa ufanisi na hatimaye kufanikisha malengo yaliyowekwa na serikali.
“Lengo la mafunzo haya ni kuongeza tija na ufanisi katika taasisi mnazozisimamia,” amesema Mchechu.
Mafunzo hayo ya siku tatu yameandaliwa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Msajili wa Hazina na Taasisi ya Uongozi, kwa lengo la kuwajengea uwezo watendaji wakuu wapya ili watekeleze majukumu yao kwa weledi na kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.
Kwa mujibu wa Mchechu, mafunzo hayo yanatolewa kwa watendaji wakuu walioteuliwa kuanzia mwaka 2022 hadi 2024; na yanafanyika kila baada ya miezi sita.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, hapa nchini, kuna taasisi, mashirika ya umma na wakala wa serikali 309 ambazo thamani ya uwekezaji wake ni Sh. 75.8 tirioni.