Serikali yaanza kujenga maabara za Kisasa Kilimanjaro,Shule elfu nne kunufaika

Wakati sayansi na teknolojia ikikuwa kwa kasi nchini, serikali imeanza utekelezaji wa ujenzi wa maabara za kisasa za Teknolojia, habari na mawasiliano(Tehama) mkoani Kilimanjaro, lengo likiwa ni kuongeza idadi ya vijana watakaoweza kushindana kwenye uchumi wa kidigitali.

Maabara hizo za kisasa zitajengwa katika shule za sekondari zaidi ya 4000 ikiwemo za kata, katika mikoa ya Kilimanjaro, Lindi,Tanga, Arusha Mwanza, Dodoma, Mbeya, Dar es salaam na Zanzibar.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa jengo la maabara ya Tehama ya kisasa iliyojengwa katika shule ya Sekondari Manushi, wilaya ya Moshi, mkoani hapa, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama nchini, Dk Nkundwe Mwasaga amesema uwepo wa maabara hizo utaleta chachu na Mapinduzi makubwa katika maendeleo ya kidigitali kwa vijana.

“Tumefanikiwa kuleta tehama kwenye ngazi ya kijiji na hii itasaidia kupata rasilimali watu na vipaji vya vijana ambao wanaweza kutoa bunifu mpya ambazo hazijawahi kutokea, tunaamini maabara hii itatoa vijana wengi ambao wanaweza kuleta Mapinduzi makubwa katika uchumi wa kidigitali,”alisema Dk Mwasaga

Alisema Tume hiyo, ipo tayari kuhakikisha Teknolojia hiyo inakuwa na inatumika sehemu nyingi ili iweze kuleta tija katika jamii ya Watanzania.

“Hii maabara ni jambo ambalo tumekuwa tukijadili sana, kwamba hii tehama tunawezaje kuifikisha kwenye misingi ya chini, maana tunaamini vipaji vingi vinatoka chini na uchumi wa kidigitali wenyewe unajengwa na vipaji,”alisema na kuongeza

“Tunaamini vijana watakaopitia darasa hili watakuwa ni chachu na ndio hao tunaowategemea serikalini kwa kufanya bunifu mbalimbali, kutoa huduma mbalimbali za Tehama na kuweza kufanya Tanzania iwe shindani katika uchumi wa kidigitali, Kikanda, Afrika na ikiwezekana dunia nzima,”alisema Dk Mwasaga

Profesa Said Vwai, ambaye ni mdau wa elimu ya sayansi nchini, alisema uanzishwaji wa maabara hizo utaleta chachu ya mabadiliko na ufaulu katika masomo ya sayansi na kuwafanya vijana kupenda masomo hayo kwa kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji.

“Kama tunavyofahamu, Tanzania kwa ujumla wake tunachangamoto kubwa sana ya vijana wetu kwenye ufaulu wa masomo ya Sayansi hasa kwenye hisabati, hivyo naamini maabara hii itakuwa ni chachu na itawasaidia sana, kwanza kuongeza hamasa,”alisema Dk Mwasaga

Aliongeza”Vijana wetu sasa hivi ni wazi kabisa wanapenda teknolojia na tunapochanganua masomo ya sayansi na teknolojia itaongeza hamasa ya kupenda masomo ya sayansi na kuongeza ufaulu wao,”alisema Dk Vwai

Naye, Mkuu wa shule hiyo, Hamis Mbawa alisema uwepo wa mradi huo wa maabara utarahisisha shughuli nzima ya utoaji wa elimu kwa haraka na kwa ufanisi mkubwa.

Pia, alisema ujenzi huo uliogharimu zaidi ya Sh 52 milioni utasaidia wanafunzi kupata uelewa na ujuzi wa Tehama, kufundishiwa na kujifunzia kwa kutumia vifaa vya tehama ambavyo vitachangia uelewa kwenye masomo na namna ya kukabiliana na maisha bora ya maisha.

Related Posts