Dar es Salaam. Wakati hali ya upepo mkali ikiendelea kushuhudiwa katika baadhi ya mikoa ya ukanda wa Pwani na Kusini unaosababishwa na kimbunga Hidaya, Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) imesema mvua zinatarajia kunyesha katika maeneo mbalimbali kuanzia usiku wa leo.
Taarifa ya TMA ya saa 24 zijazo imeonyesha mikoa 20 inatarajiwa kupata mvua kuanzia saa tatu usiku wa leo.
Taarifa hiyo iliyotolewa leo Ijumaa Mei 3, 2024 imeitaja mikoa inayotarajiwa kupata mvua kubwa ni Lindi, Mtwara, Dar es Salaam na Unguja.
Mikoa mingine ni Ruvuma, Kigoma, Geita, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Simuyu, Mara, Arusha, Manyara Kilimanjaro, Pwani, Morogoro, Tanga na mikoa ya Pemba.
Hili linakuja ikiwa zimepita siku chache tangu mikoa mbalimbali nchini ipate mafuriko kufuatia mvua kubwa zilizosabisha uharibifu wa miundombinu na takribani watu 155 kupoteza maisha.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya TMA, vinatarajiwa vipindi vya upepo mkali unaofikia kilomita 60 kwa saa na mawimbi makubwa yanayozidi mita mbili hasa katika maeneo ya ukanda wa Pwani, hivyo watu wametakiwa kuchukua tahadhari.
Kufuatia hali hiyo TMA imetahadharisha upo uwezekano wa baadhi ya makazi kuzungukwa na maji, kuathirika kwa shughuli za baharini na uharibifu wa miundombinu ya bahari.
Kuhusu kimbunga Hidaya, mamlaka hiyo imeeleza kuwa kimeendelea kuimarika na kusogea kuelekea maeneo ya pwani ya nchi, umbali wa takribani kilomita 342 Mashariki ya pwani ya Mtwara.
“Katika kipindi hicho kimbunga Hidaya kimeendelea kuimarika zaidi huku kasi ya upepo ikiongezeka hadi kufikia kilomita 140 kwa saa,” imeeleza taarifa hiyo.
Hata hivyo, taarifa za ufuatiliaji TMA imesema zinaonesha upo uwezekano wa kimbunga hicho kupungua nguvu kwa kiasi kwa saa 12 zijazo, huku kikitarajiwa kuendelea kuwepo hadi Mei 5 na kasi yake kupungua kuanzia siku hiyo.
Msemaji wa Serikali atoa tahadhari
Kwa upande wake,Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema kimbunga hicho kinaendelea kupungua kasi na huenda saa 12 zijazo kitakuwa kimepungua zaidi, huku akiitaja mikoa ya Lindi na Mtwara kuwa imekwishaanza kupata athari.
“Lakini pia madhara ya kimbunga hicho yameanza kuonekana kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara kwani kumekuwepo na mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali unaovuma kwa kasi ya kilomita 40 kwa saa,” amesema Matinyi.
Aidha, Matinyi amesema Serikali inawataka wakazi wote wa maeneo hayo wanaojishughulisha na shughuli za baharini kuchukua tahadhari.
“Kutokana na hali hiyo mamlaka imeshauri wananchi wa mikoa husika na wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali baharini kuchukua tahadhari na kufuatilia taarifa za TMA,” amesema Matinyi.