Balozi Dk Nchimbi ameongeza kusema kuwa katika kutekeleza kwa vitendo Falsafa ya 4R ya Mhe. Rais Samia na kuwatumikia wananchi waliokipatia dhamana ya kuongoza, CCM kikiwa Chama kiongozi nchini, kitaendelea kutimiza wajibu wake wa kuwaunganisha Watanzania kuwa wamoja wenye mshikamano bila kubaguana kwa kuangalia maeneo wanayotoka, dini, kabila wala itikadi za kisiasa.
Balozi Dkt Nchimbi, ameyasema hayo wakati wa mazungumzo kati yake na Katibu Mkuu wa Chama Tawala cha Burundi, CNDD – FDD, Mhe. Révérien Ndikuriyo, yaliyofanyika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Mtaa wa Lumumba, jijini Dar Es Salaam, leo Ijumaa, Mei 3, 2024.
“Asante kwa pongezi zako za utekelezaji wa ilani ya CCM. Mojawapo ya nguzo za uimara wa CCM ni pamoja na kazi kubwa sana zilizofanywa na Serikali ya CCM chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ndani ya miaka hii mitatu. Zinatupatia ujasiri na jeuri ya kuwa barabarani, kwenda kuzungumza na wananchi kwa sababu tunayo mambo ya kusema na kuonesha. Na wananchi wanatuunga mkono.
“Lakini pia katika uhusiano kati yetu, CCM tunafurahi sana jinsi ambavyo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Burundi, Mheshimiwa Évariste Ndayishimiye ni marafiki. Hivyo vyama vyetu ni marafiki, nchi zetu ni rafiki na hata viongozi wetu ni marafiki, ni wajibu wetu sisi tuendelee kuenzi na kulinda uhusiano na ujirani wetu mwema, kwa ajili ya watu wetu wa pande zote mbili,” amesema Balozi Dk Nchimbi.
Kwa upande wake Mhe. Ndikuriyo amesema kuwa CCM na Tanzania kwa ujumla, ni sehemu muhimu kujifunza kwa ajili ya kujiimarisha, hususani wakati huu ambapo Chama cha CNDD – FDD kinaendelea kuisimamia Serikali ya Burundi katika kulinda misingi ya demokrasia inayotokana na utashi wa Warundi.
Katika ujumbe wake, Mhe. Ndikuriyo aliambatana na
Balozi wa Burundi nchini Tanzania, Mhe. Leontine Nzeyimana na maofisa wengine wa Chama cha CNDD – FDD kutoka Burundi.