Mafunzo ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Yaleta Mabadiliko katika Uelewa wa Jamii

NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

TUME ya Taifa ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imeombwa kutoa elimu kwa umma kuhusu Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ili kuongeza uelewa katika jamii.

Ombi hilo limetolewa leo Oktoba 9,2024 Jijini Dar es Salaam,katika mafunzo ya kukuza uelewa wa sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi ambayo yamefanyika kwa siku mbili kuanzia Oktoba 8 -9 , 2024 yakiwakutanisha wadau mbalimbali nchini na nje ya nchi.

Katika warsha hiyo, Afisa Mradi wa Shirika la The Paradigm Initiative , Miriam Wanjiru, amesisitiza umuhimu wa tume hiyo kuwa huru na isiyoingiliwa na serikali, ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa maslahi ya taifa kwa ujumla. 

Amesema kuwa serikali inawajibu wa kuwaelimisha wananchi kuhusu sheria hiyo ili kulinda faragha zao.

“Katika nchi nyingine nilizopita nimeshuhudia mashirika yakiwafundisha watu mbalimbali kuanzia ngazi ya shina yakijengea uelewa kwa kina kuhusu Sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi, na muitikio unaridhisha”. Amesema 

Kwa upande wake Mratibu wa Kitaifa Mtandao wa Mashirika ya binadamu Kusini mwa Afrika (SAHRiNGON) Martina Kabisama amesema kuna umuhimu mkubwa hasa katika ulimwengu huu wa utandawazi watu wakaelewa umuhimu wa ulinzi wa taarifa binafsi.

Ameeleza kuwa baada ya warsha hiyo, atakutana na asasi za kiraia ili kujua uelewa wao kuhusu ulinzi wa taarifa binafsi na kutafuta njia za kuwafikia wananchi kwa ujumla.

Pamoja na hayo Kabisama amesema anaamini watu wataelewa  kwa undani kuhusiana na Sheria hiyo ya haki taarifa binafsi ambapo wataanza kutumia inapotokea wanaona kuna mambo hayaendi sawa.










Related Posts