Matukio ya ubakaji yazidi kutikisa Mwanza

Mwanza. Kutokana na hali kuendelea kuwa mbaya ya ukatili wa kijinsia nchini, imeelezwa kuna haja ya kuendelea kutoa elimu ya kina kwa wananchi ya namna ya kuzuia matukio hayo yasiendelee kutokea.

Katika Mkoa wa Mwanza pekee, imeelezwa matukio ya ubakaji yanazidi kuongezeka na mpaka sasa, matukio 537 yameripotiwa katika kipindi cha miaka miwili kuanzia 2022 hadi Aprili 2024.

Yanafuatiwa na ya mimba ambazo jumla ya wanafunzi 534 wameripotiwa kubeba ujauzito wakiwa suleni kwa kipindi kama hicho.

Akizungumza leo Mei 3, 2024 wakati wa uzinduzi wa jengo la dawati la jinsia na watoto Wilaya ya Nyamagana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa ametaja matukio mengine yaliyoongoza kuwa ni ulawiti 197, ukatili kwa watoto 160, utelekezaji wa familia 131, utoroshaji wa wanafunzi 69, utupaji watoto 43, wizi wa watoto 35 na kuzini mahalimu 16.

“Matukio ya ubakaji kwa mwaka 2022 yaliripotiwa 235, 2023 matukio 254, na Januari hadi Aprili mwaka huu 48 tunapotaja idadi hii tuna maanisha wale wote walioathirika na waliokamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria na hatua kuchukuliwa,” amesema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa jengo la dawati la jinsia na watoto Wilaya ya Nyamagana. Picha na Anania Kajuni

Amesema matukio ya ulawiti kwa mwaka 2022 yalikuwa 91, mwaka 2023 yalikuwa 84 na Januari mpaka Aprili mwaka huu yalikuwa 22. Kutupa watoto kwa mwaka 2022 yalikuwa 16, mwaka 2023 yalikuwa 19 na mwaka huu katika kipindi cha miezi minne yalikuwa manane.

“Wizi wa watoto kwa mwaka 2022 yalikuwa matukio 16 na mwaka 2023 yalikuwa 16 na mwaka huu matatu,” amesema.

“Kuzini mahalimu matukio nane mwaka 2022, 2023 matukio nane na mwaka huu tayari yako mawili. Kutelekeza familia 2022 matukio 68, 2023 matukio 48 na katika kipindi hiki cha miezi minne 15. Utoroshaji wanafunzi matukio 31 mwaka 2022, 30 mwaka 2023 na matukio nane mwaka huu,” amesema Kamanda Mutafungwa

Matukio mengine ni mimba kwa wanafunzi mwaka 2022 yalikuwa 285, mwaka 2023 matukio 195 na mwaka huu 54 huku ukatili wa watoto mwaka 2022 ukiwa 72, 2023 matukio 63 na mwaka huu matukio 25.

Hata hivyo, amesema; “Uwepo wa jengo hili la dawati la jinsia na watoto linaenda kutoa nafasi kwa mwathirika wa vitendo vya ukatili kueleza taarifa zake kwa usiri, faragha na utulivu mkubwa lakini pia kulinda ushahidi, kutoa ushauri na huduma ya kwanza,” amesema Mutafungwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kivulini, Yassin Ally amesema ili kupunguza matukio hayo ya ukatili madawati hayo nchini yanatakiwa kuanza kutoa elimu na huduma tembezi kuhusu ukatili katika jamii.

“Kupitia uzinduzi wa jengo hili niombe Jeshi la Polisi nchini liboreshe madawati mengine kama haya katika mikoa mingine lakini pia nashauri elimu na huduma kuhusu matukio haya ya ukatili iwe tembezi ili kuwafikia wananchi wengi wa vijijini,” amesema Yassin

Akizungumzia kuhusu jengo hilo ambalo limejengwa kwa zaidi ya Sh65 milioni kwa fedha za wadau na wananchi huku Shirika la SOS Children’s Villages likichangia zaidi ya asilimia 83, Mratibu wa Mpango wa Kuimarisha Familia Kutoka Shirika la SOS Children’s Villages, Elizabeth Swai amesema kutokana na matukio mengi ya ulawiti kufanywa na ndugu, ameiomba jamii kutumia dawati hilo kuripoti matukio hayo kwa usiri na ushirikiano mkubwa.

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi ametoa wito kwa jamii kuungana kwa pamoja katika kupambana na vitendo vya ukatili ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa katika madawati hayo.

“Saizi tunahitaji kuwa na elimu inayotembea ya kutoa ukatili sasa tunapozindua jengo letu hili nitoe wito kwa wananchi tukubali na tuamue kuwa vitendo hivi haviwezekani na havikubaliki katika jamii yetu,” amesema Makilagi

Mmoja ya washiriki katika hafra hiyo ambaye pia ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut) Mwanza, Samia Mussa amelipongeza jeshi hilo kwa kuzindua jengo hili ambalo anaamini litasaidia kupunguza matukio ya ukatili mkoani humo.

Related Posts