Dar es Salaam. Chama cha ACT- Wazalendo kimetoa mapendekezo mbalimbali kwa Serikali ya Tanzania ili kuboresha sekta ya kilimo ikiwemo kuweka mfumo wa kodi unaoeleweka utakaohakikisha mkulima anabaki na sehemu kubwa ya mapato baada ya kuuza mazao yake.
Mbali na hilo, chama hicho kimeishauri pia Serikali kupunguza utitiri wa kodi, ushuru na tozo kwenye mazao.
Mapendekezo hayo yametolewa leo Ijumaa Mei 3, 2024 na Waziri Kivuli wa Kilimo, Umwagiliaji na Maendeleo ya Ushirika wa chama hicho, Mtutura Abdallah wakati akiichambua bajeti hiyo iliyowasilishwa jana Alhamisi Mei 2, 2024.
Jana Alhamisi, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe aliliomba Bunge liidhinishe Sh1.248 trilioni zitakazotumika kwenye vipaumbele sita vyenye mikakati 27 katika mwaka wa fedha wa 2024/2025.
Mtutura amesema kumekuwa na changamoto ya kushuka kwa bei za mazao ya wakulima nchini, kutokana na kukosekana kwa mfumo wa kodi unaoeleweka katika kusimamia sekta ya kilimo na kurudisha nyuma maendeleo ya wakulima.
Mtutura aliyewahi kuwa mbunge wa Tunduru, mkoani Ruvuma amesema kuporomoka kwa bei ya mazao ya wakulima kunasababisha kundi hilo, kutoona tija ya jasho lake.
Msemaji huyo wa sekta ya kilimo, amesema chama hicho hakijaridhishwa na usimamizi wa sekta hiyo, ili kufikia malengo ambayo Serikali ilijiwekea ifikapo mwaka 2030, kuwa kilimo kutakua kufikia asilimia 10.
“Tanzania haiwezi kuondoa umaskini kwa kauli mbiu tu bali kuwa na maono wa uwazi katika mipango ya kilimo hivyo wanahitaji uchumi wa nchi ukue kwa kasi ya wastani wa asilimia nane kwa mwaka,” amesema Mtutura.
Katika mkutano huo, Mtutura tathmini ya uzalishaji wa mazao ya chakula nchini mwaka 2021/2022 akisema kwa mujibu wa taarifa za wizara hiyo, umeshuka hadi kufikia tani milioni 17.1 kutoka tani milioni 18 za msimu wa mwaka 2020/2021.
Mtutura amesema uzalishaji wa mazao ya chakula umeshuka kwa asilimia 15, upungufu huo una mchango mkubwa kwenye kuathiri mwenendo wa bei za vyakula na kuwepo kwa uhaba wa chakula nchini.
Jana akiwasilisha bajeti hiyo ya Kilimo ambayo imepitishwa na Bunge leo, Waziri Bashe alisema kwa msimu wa kilimo wa 2022/2023 uzalishaji ulitosheleza mahitaji ya chakula ya tani 16,390,404 kwa mwaka 2023/2024 na kuwepo kwa ziada ya tani 4,011,611.
“Kutokana na hali hiyo, Taifa limejitosheleza kwa chakula kwa asilimia 124 ikilinganishwa na utoshelevu wa asilimia 114 mwaka 2022/2023,” alisema.
Alisema utoshelevu wa chakula unatarajiwa kufikia asilimia 130 ifikapo mwaka 2025.