Mkazi wa kijiji cha Luchima katika kata ya Majimoto halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi Bw. Aseni Jandikile ametoa shilingi elfu tano kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Dkt Samia Suluhu Hassan kutokana na juhudi zake za kuwaletea maendeleo wananchi.
Kiasi hicho cha pesa kimekabidhiwa kwa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Jimbo la Kavuu Mhe, Geophrey Pinda tarehe 3 Mei 2024 wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Luchima alipokwenda kuzungumza nao wakati wa ziara yake ya kuwafariji wananchi waliopatwa na mafuriko katika jimbo lake la Kavuu.
‘’Nampongeza rais kwa vitendo kabisa naomba mhe, mbunge leo nikikabidhiwa fedha taslimu shilingi elfu tano umpelelekee Mhe, Rais ’’ alisema.
Kwa mujibu wa mwananchi huyo, uamuzi wake unatokana na kuwiwa na uongozi bora na utendaji kazi wa Rais Samia hasa kwa kuwajali wananchi wa Luchima ambapo mbali na mambo mengine amewajali kwa kutoa fedha milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati aliyoieleza imewakomboa wananchi wa kijiji hicho.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Jimbo la Kavuu Mhe, Geophrey Pinda amesema atahakikisha kiasi hicho cha fedha kilichotolewa na mwananchi huyo kinamfikia mhe, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Amempongeza mwananchi huyo wa kijiji cha Luchima wa uamuzi wake wa kutoa kiasi hicho cha fedha kama ishara ya kukubali juhudi na kazi kubwa inayofanywa na Mhe, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Luchima na Tanzania kwa ujumla.
Amewaaleleza wananchi wa kijiji hicho kuwa, Rais Samia anawapenda sana na amekuwa akisaidia juhudi mbalimbali za maendeleo kwenye jimbo la Kavuu na kutaja baadhi ya juhudi hizo kuwa ni pamoja na kutoa fedha za ujenzi wa hospitali, shule, barabara pamoja na upatikanaji wa huduma za maji.
Mhe, Pinda amefanya ziara katika jimbo lake la Kavuu kuwafariji wananchi waliopatwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa na kuathiri miundiombinu ikiwemo madaraja.