Ripoti iliyotolewa na shirika la Mtoto Initiative inasema ustawi wa mtoto wa kike nchini unazidi kuporomoka ndani ya miaka mitano hatua inayozua wasiwasi.
Ripoti inasema kiwango cha watoto wanaopata mimba licha ya kuwepo juhudi mbalimbali kukabili hali hiyo bado kiko juu.
Wataalamu walioandaa ripoti wanabainisha kuwa, mazingira jumla kwa mtoto wa kike nchini Tanzania siyo rafiki akilazimika kuruka viunzi vya aina mbalimbali ikiwemo vile vitokanavyo na mtanzuko wa kimazingira kama vile vilivyomo ndani ya familia.
Ukosefu wa fursa za elimu
Kukosekana kwa haki na usawi kwa makundi mengi ya watoto ni eneo lingine llinaloendelea kuwa ndonda ndungu hali ambayo imesababisha madhila yake kuwa mtambuka.
Hali hiyo kama inavyobainishwa na mtafiti Rebbeca Gyumi imesababishwa na ongezeko la matukio kama vile yale yanayohusiana na ukatili wa kingono.
Ukosefu wa fursa za elimu ni mwiba mwingine ambao bado unazidi kurudisha nyuma ustawi wa watoto wengi wa kike hasa wale wanakutikana maeneo ya vijijini ambako ukumbatiaji wa mila potufu bado unaendelea kushamiri katika baadhi ya maeneo.
Ingawa serikali imechukua mkondo wa kulia kupanua fursa za kielemu kwa kuendelea na ujenzi wa shule mbalimbali, hata hivyo watoto wengi wa kike bado wanaendelea kuogelea katika lindi la ukosefu wa elimu.
Mkuu wa shirika hilo la Msichana Initiative, Gyumi anasema kuna mengi yanayowafanya wasichana hao kutofikiwa na fursa hiyo.
Pamoja na jitihada kubwa zinazosukumwa na mashirika ya kiraia kwa kuungwa mkono na mamlaka za kiutendaji, takwimu nyingi kutoka duru za kimataifa zinaonyesha watoto wa kike bado wanakabiliwa na safari ndefu kufikia ustawi wao.
Kongamano la watoto wa kike
Mtaalamu Fundikira Wazambi aliyeshiriki katika utafiti kuhusu ustawi wa watoto wa kike anasema, kuna uwezekano mkubwa hali hiyo ni sehemu ya matokeo ya mfumo dume ambao unaanza kumea mizizi kuanzia ngazi ya familia na baadaye kuendelea hata katika mashule.
Kama hatua mojawapo ya kukabiliana na madhila yanayoendelea kuwaandama, watoto wa kike kote nchini Ijumaa watakuwa katika kongamano maalumu wakiwa katika mwavuli ujulikanayo ajenda ya msichana wakichambua na kusaka mbinu za njinsi ya kuvuka vizingiti hivyo.
Mtaalamu wa eneo hilo, Furahia Michael anasema jukwaa hilo linamulika maeneo mbalimbali yanayowatatiza wasichana lakini safari hii kipaumbele zaidi kitazingatiwa katika maeneo mawili ikiwamo lile linalogusa uongozi.
Desemba 19, 2011, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio maalumu na kutangaza Oktoba 11 kama Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike ikiweka vipamble vitavyomwezesha mtoto huyo kuondokana na changamoto zinazomkabili.