Tumieni Fursa hii ya kuonana na madaktari bingwa – Dr. Nkungu

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro Dkt. Daniel Nkungu amewataka wananchi wa Mkoa wa huo kutumia fursa iliyotolewa sasa kujitokeza kwa wingi katika hopsitali hiyo kwa ajili ya kuonana na madaktari bingwa kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI).

Dkt. Nkungu amebainisha hayo wakati akiongea na waandishi wa habari kwa lengo la kutoa taarifa ya uwepo wa madaktari hao bingwa Mkoani Morogoro na hiyo itaanza kutolewa kuanzia Oktoba 15 hadi 19, 2024 katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Morogoro ikiwa ni sehemu ya kumbukizi ya kifo cha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Dkt. Nkungu amesema matibabu hayo yataongozwa na madaktari bingwa kutoka MOI wakishirikiana na madaktari bingwa wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro na kwamba huduma ya kumuona daktari itatolewa bila malipo

Kwa sababu hiyo amewataka wananchi wa Mkoa wa Morogoro na Mikoa ya jirani kutumia fursa hiyo kufika na kuonana na madaktari hao bingwa ili kupata tiba za kibingwa.

“.. niwaombe na kuwashauri wananchi wote wa Mkoa wa Morogoro na Mikoa jirani kutumia fursa hii adhimu kuonana na madaktari bingwa na wabobezi kwa ajili ya kupata matibabu…” amesisitiza Dkt. Daniel Nkungu.

Aidha Dkt. Nkungu amebainisha magonjwa ambayo yatatibiwa kuwa ni ni pamoja na watu wenye matatizo ya mivunjiko ya mifupa, matatizo ya nyonga, magoti, mgongo, kiharusi, ubongo, mishipa ya fahamu, watoto wenye ulemavu na mguu kifundo, kibiongo, mgongo wazi na vichwa vikubwa.

Kambii hii ya madaktari bingwa na wabobezi ni utekelezaji wa agizo la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kusogeza huduma za kibingwa na kibobezi karibu na wananchi.

 

 

Related Posts