Dar/Unguja. Kutokana na hali mbaya ya hewa baharini, safari za boti kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar na vivuko mbalimbali vimesitishwa hadi Jumatatu ya Mei 6, 2024 huku abiria waliokuwa wamekata tiketi wakirudishiwa nauli zao.
Safari hizo zimesitishwa kutokana na tahadhari iliyotolewa kwa baadhi ya mikoa nchini kutarajiwa kukumbwa na Kimbunga Hidaya.
Tahadhari hiyo ilitolewa kwa mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Pwani, Tanga, Morogoro na visiwa vya Unguja na Pemba kuwa inatarajiwa kukabiliwa na Kimbunga Hidaya kwa siku tano mfululizo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kimbunga hicho, kitakuwa kikubwa zaidi kutokea nchini Tanzania, ukiachana na kile kilichotarajiwa kutokea mwaka 2019 kilichokuwa na umbali wa kilomita 237 kutokea Msumbiji, lakini baadaye kilitoweka.
Kutokana na hali hiyo, mamlaka hiyo ilishauri wa mikoa husika na wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali baharini, kuchukua tahadhari na kufuatilia taarifa za TMA.
Mwananchi Digital imefika katika Bandari ya Dar es Salaam leo asubuhi Jumamosi Mei 4, 2024 na kushuhudia abiria waliokuwa katika Boti ya Kilimanjaro wakishuka na kwenda ofisi za Azam kisha wamerudishiwa nauli zao.
Msimamizi wa operesheni za abiria boti za Kilimanjaro, Said Salum amesema wamepokea maelekezo asubuhi ya leo kusitisha safari zote hadi Jumatatu.
“Wakati abiria wanajiandaa kuondoka, tumepokea maelekezo kutoka mamlaka kusitisha safari kutokana na hali mbaya ya hewa hadi keshokutwa (Jumatatu), hivyo tunawarudishia abiria waliokuwa wamekata tiketi nauli zao,”amesema Salum.
Wakizungumza kusitishwa kwa safari baathi ya abiria wamesema kutawaathiri kutokana na majukumu waliyokuwa wanawahi huku wengine wakisifu hatua hiyo.
Amina Salum amesema alikuja Dar es Salaam kwa ajili ya shughuli hivyo alikuwa akirejea Unguja kwenye familia yake.
“Nimekuja Dar es Salaam tangu juzi, nilikuwa na shughuli na leo nilikuwa nawahi familia yangu kwa ajili ya maaandalizi ya watoto shule Jumatatu, lakini baada ya kukata tiketi na kuingia kwenye boti tumeaambiwa kutokana na hali mbaya ya hewa safari zimesitishwa hadi Jumatatu,” amesema Amina.
Mfanyabiashara wa filamu, Athuman Issa amesema kusitishwa kwa safari hizo kutamuathiri kutokana na ratiba aliyokuwa ameipanga huku akiipongeza mamlaka husika kuwa imetumia busara kwa kuthamini uhai wa watu.
“Ni kweli fedha inatafutwa lakini uhai ni bora zaidi, ingawa kusitishwa kwa safari kutaniathiri lakini mimi naona ni bora kuliko madhara yanayoweza kujitokeza,” amesema Issa.
Tahadhari imeendelea kuchukuliwa huku Serikali ya Zanzibar ikisitisha usafiri wa vyombo vyote vya baharini kutoka Unguja kwenda Dar es Salaam, Pemba na Tanga kutokana na upepo mkali uliosababishwa na Kimbunga Hidaya.
Katika visiwa vya Zanzibar, upepo mkali ulianza kuvuma saa 3:00 usiku jana Ijumaa Mei 3, 2024 mpaka sasa unaendelea katika maeneo yote ya kisiwa hicho.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumamosi Mei 4 2024, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usarifi Baharini Zanzibar (ZMA), Sheikha Ahmed Moh’d amesema wamesitisha usafiri huo vyombo vyote vya baharini.
“Hali sio nzuri kutokana na utabri tuliopata kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), na hivi sasa tumezuia vyombo vyote hakuna kusafiri mpaka kesho asubuhi tutakuja kuangalia tena,” amesema Moh’d.
“Tumeshatoa taarifa na tunaendelea kutoa taarifa kwa wananchi na vyombo vyote vinavyohusika hakuna kusafiri.” amesema.
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Khalid Salum Mohamed amesema kutokana na upepo mkubwa uliovuma usiku kucha tayari zimechukuliwa tahadhari.
“Tunasitisha usafiri wote wa baharini, kutoka Unguja kwenda Dar es Salaam, kutoka Pemba kweda Tanga na kutoka mpaka kesho asubuhi tuone hali itakavyokuwa,” amesema Waziri Mohamed.
Kuhusu upande wa viwanja vya Ndege, Waziri Mohamed amesema bado wanafuatilia; hali itakavyokuwa watazungumza na wananchi.
“Kwa viwanja vya ndege kuna mamlaka zinazotushauri sasa tutaangalia wanasemaje,” amesema Mohamed.
Mwanachi Digital imeshuhudi baadhi ya abiria wakiwa tayari Bandari ya Malindi wakirejea nyumbani kutokana na kusitishwa safari za boti.
Amani Mageta, mkazi wa Chato Geita, amesema hali hiyo imemuathiri kwa kuwa muda wa kukaa Zanzibar umeisha alitakiwa kuondoka huku akidai hana fedha ya kuendelea kujikimu.
Abiria mwingine Salma Hussein amesema iwapo walijua watasitisha usafiri huo wasingekatisha tiketi.
Temesa yazuia vivuko vyote
Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa) umetangaza kusitisha huduma za vivuko katika mikoa mitatu ya Mtwara, Lindi na Pwani kufuatia tahadhari iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu uwapo wa kimbunga Hidaya.
Temesa imesema hayo jana Ijumaa Mei 3, 2024 kupitia barua kwa umma iliyotolewa na Kitendo cha Masoko na Uhusiano cha wakala huo.
“Kutokana na kuwepo kwa tahadhari hiyo, Temesa inawajulisha watumiaji wa vivuko kuwa katika baadhi ya maeneo ya Mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia, mikoa ya Dar es Salaam na Tanga kwamba kutakuwa na kusimama kwa utoaji wa huduma ya vivuko ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza,” imesema taarifa hiyo.
Taarifa ya leo Jumamosi ya TMA inasema hadi kufikia saa 9 usiku wa kuamkia leo, mwenendo wa Kimbunga Hidaya kilikuwa eneo la bahari takriban kilomita 125 kutoka pwani ya Kilwa (Mkoa wa Lindi), kilomita 93 kutoka pwani ya Mafia na kilomita 128 kutoka pwani ya Dar es Salaam kikiwa na mgandamizo wa hewa wa kiasi cha 985 hPa na kasi ya upepo unaofika kilomita 120 kwa saa.
Kwa mujibu wa TMA uwepo wa Kimbunga Hidaya karibu kabisa na pwani ya Tanzania umeendelea kutawala mifumo ya hali ya hewa katika maeneo hayo, katika kipindi cha saa 6 zilizopita, vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali vimeendelea kujitokeza.
Taarifa hiyo inatolea mfano kuwa, katika vituo vya hali ya hewa vya Mtwara, Kilwa, Zanzibar na Dar es Salaam upepo mkali unaozidi kilomita 50 kwa saa umeweza kupimwa katika nyakati tofauti kuanzia usiku wa kuamkia leo hadi asubuhi hii.
Pia, inaeleza katika kipindi hicho, vipindi vya mvua kubwa vimeendelea kushuhudiwa katika maeneo ya Mtwara na Lindi na hadi kufikia saa 9 usiku kituo cha Mtwara kiliripoti jumla ya milimita 75.5 za mvua ndani ya saa 12.
Inaeleza kuwa, kiwango hiko cha mvua ndani ya saa 12 ni kikubwa sana ukizingatia kuwa wastani wa mvua kwa Mei kwa kituo cha Mtwara ni milimita 54 tu. Hivyo kiasi cha mvua kilichonyesha ndani ya saa 12 katika kituo cha Mtwara ni takribani asilimia 140 ya wastani wa mvua kwa Mei kwa kituo hicho.
Aidha, Kimbunga Hidaya kinatarajiwa kuendelea kusogea karibu zaidi na ukanda wa pwani ya Tanzania huku kikipungua nguvu yake taratibu kuelekea usiku wa kuamkia kesho Mei 5, 2024.
Imeandikwa na Fortune Francis (Dar), Jesse Mikofu na Muhamed Khamis (Unguja)
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa mbalimbali