MAHAKIMU WAKAZI RUVUMA WAPATA MAFUNZO YA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA

 

Na Albano Midelo,Songea

Mahakama Kuu Kanda ya Songea  imetoa mafunzo ya uchaguzi wa serikali za mitaa kwa waheshimiwa mahakimu wakazi kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma.

Mafunzo hayo ya siku moja yamefanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Huntlcub Ruhuwiko mjini Songea,yamefunguliwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea Mheshimiwa James Karayemaha.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo,Jaji Mheshimiwa Karayemaha amesema Mahakama hiyo iliandaa sera ya mafunzo ya mwaka 2019 kwa lengo la kushusha mafunzo kwenye Kanda hiyo.

Amesema mafunzo hayo yameandaliwa kama sehemu ya utekelezaji wa sera hiyo ambayo yatawajengea uwezo   waheshimiwa mahakimu kufahamu sheria mbalimbali zinazohusiana na uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa kwa mwaka 2024.

“Mafunzo ya uchaguzi wa serikali za mitaa ,yatawasaidia kujua sheria,kanuni na taratibu zinazoongoza uchaguzi,yatasaidia kujua namna bora ya kupokea ,kusikiliza na kuamua migogoro ya aina yoyote itakayoletwa mbele ya mahakimu’’,alisisitiza.

Hata hivyo ameutaja uchaguzi wa serikali za mitaa ni suala muhimu katika ustawi wa demokrasia nchini ambapo waheshimiwa mahakimu wote  wa Tanzania ni sehemu ya mchakato wa kufanikisha uchaguzi wa serikali za mitaa ambao ni makamishina wa viapo.

Amewataja waheshimiwa mahakimu kuwa ndiyo  watakaowaapisha wasimamizi wa uchaguzi na viongozi watakaochaguliwa kabla ya kuanza rasmi kufanya shughuli zao kwa mujibu wa sheria.

Katika hatua nyingine Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea  amewahimiza watumishi wa Mahakamu kufanya kazi kwa kusikiliza na kutoa maamuzi kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA  hivyo kuachana na matumizi ya karatasi.

Kwa upande wake Mwezeshaji wa mafunzo hayo Hakimu Mkazi Mfawidhi,Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Songea Mheshimiwa Japhet Manyama amesema mafunzo hayo yanatolewa kwa waheshimiwa mahakimu kwa lengo la kuwaandaa kwa ajili ya  kusikiliza na kuamua mashauri yatakayotokea wakati wa  uchaguzi wa serikali za mitaa.

Amelitaja lengo kuu la mafunzo hayo kuwa ni kuwaandaa na kuwapitisha mahakimu katika sheria zinazohusu uchaguzi zikiwemo kanuni  zinazotumika kwenye uchaguzi wa serikali  za mitaa na kuwaandaa namna ya kumudu msukumo wa kisiasa na jamii kwa kuangalia sheria ili waweze kutoa  maamuzi ya haki kwa wote.Jaji Mfawidhi wa Mahakamu Kuu Kanda ya Songea Mheshimiwa James Tarayemaha akiwa katika picha ya pamoja na waheshimiwa mahakimu wa Mkoa wa Ruvuma kwenye mafunzo ya uchaguzi wa serikali za mitaa yaliyofanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Huntklub mjini SongeaJaji Mfawidhi wa Mahakamu Kuu Kanda ya Songea Mheshimiwa James Tarayemaha akizungumza wakati anafungua mafunzo ya uchaguzi wa serikali za mitaa kwa waheshimiwa mahakimu wa Mkoa wa Ruvuma.Baadhi ya waheshimiwa  mahakimu wa Mkoa wa Ruvuma wakiwa katika mafunzo ya uchaguzi wa serikali za mitaa.

Related Posts