SIJUI kama imebadilika lakini nimekumbuka zamani. Zamani yetu shuleni. Walimu walikuwa na akili timamu kupanga tuanze na mahafali kisha twende katika mitihani. Ingewafanya wanafunzi wenye vurugu kuwa na nidhamu siku ya sherehe yao ya mwisho shuleni. Sijui nani alipata wazo lile.
Haijatokea hivyo Liverpool. Nimekumbuka Jumamosi mchana pale Uwanja wa Olimpiki London. Kulikuwa na mahafali baada ya mtihani. Liverpool wapo katika siku za mwisho za msimu wao na zama zao. Zama? Ndio, kila kitu kinakwenda mwisho. Msimu wao umefika mwisho kwa sababu inaonekana hawataondoka na kombe lolote lile. Kazi ya kuombea Manchester City na Arsenal wote wachemke katika mbio za ubingwa ni kazi ngumu.
Zama nazo zinafika mwisho wake. Sadio Mane aliondoka. Roberto Firmino aliondoka. Fabinho aliondoka. Kuna wachezaji wanakaribia mwisho.
Kuanzia Mo Salah hadi Virgil Van Dijik. Lakini zaidi, ‘sterling’ wa filamu nzima, Jurgen Klopp naye ameshatangaza kuondoka. Huu ni mwisho wa zama. Watakumbukwa milele.
Nini kilitokea London jioni ile? Ghafla tukaona Mo Salah na Klopp wakifokeana katika mstari ambao wachezaji huingilia uwanjani. Zamani isingeweza kufikirika kama mwanafunzi huyu na mwalimu huyu wangefanya haya hadharani. Hata hivyo imetokea na hii ni kwa sababu walishamaliza mitihani yao na sasa wanafanya mahafali.
Wote wawili hawaoni mbele yao Liverpool. Klopp anaondoka Anfield na nahisi Salah anaondoka pia mwishoni mwa msimu.
Niliwahi kuandika hapa hapa, simwoni Salah akipitisha siku zaidi Anfield baada ya msimu huu. Mradi wao ni kama umefika tamati na ana kila sababu ya kwenda kwa Waarabu wenzake pale Saudi Arabia. Pesa hazitakuwa kikwazo. Wanaweza kumlipa hata Pauni 500,000 kwa wiki akitaka.
Baada ya kumaliza mitihani yao iliyowakabili Anfield kwa kutwaa Ligi ya Mabingwa Ulaya, kutwaa Ligi Kuu England, kombe ambalo halikuwahi kukanyaga Anfield kwa miaka 30, ni wazi wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika mitihani iliyowakabili Anfield. Hawana deni. Hata hivyo mahafali ni wakati wa ugomvi.
Klopp ataondoka kwa sherehe na kama Salah ataondoka basi ni kwa sherehe. Hata hivyo hilo limesababisha wafunue mioyo yao, hasa kwa Salah.
Hatukuwahi kujua kama ni mtu mkorofi kiasi kile. Alificha tabia kwa sababu alikuwa katika mitihani. Sasa hivi anafunua tabia kwa sababu anajua Klopp anaondoka.
Anafahamu iwe isiwe kocha wake msimu ujao hatakuwa Klopp. Anajua Klopp anaondoka. Anajua hata akiamua kuondoka basi kokote ambako anakwenda kwa sasa kocha wake hatakuwa Klopp kwa msimu ujao. Klopp ametangaza kutofundisha soka msimu ujao kwa sababu amechoka. Hapa ndipo Salah alipopoteza nidhamu.
Unaweza kuwa umechukia kupita kiasi lakini namna gani unaweza kupoteza heshima kwa mtu ambaye alikuchukua kutoka AS Roma na kukurudisha katika Ligi kuu England huku akikugeuza kuwa mchezaji tishio zaidi duniani nyuma ya wale watawala wa muda mrefu, Cristiano Ronaldo na Lionel Messi? Kuna wakati unapaswa kurudisha moyo nyuma.
Kwa nini waligombana? Inajaribu kufichwa huku ikisemekana Salah hakutoa mkono vyema wakati Klopp alipokuwa anamwingiza uwanjani katika pambano hili dhidi ya West Ham. Vyovyote ilivyo ni wazi Salah alikuwa amechukizwa kukaa nje kwa muda mrefu katika pambano hilo. Hakujiona kama mchezaji aliyestahili kukaa benchi. Mambo yale yale ya Cristiano Ronaldo na Erik Ten Hag.
Hata hivyo, tuliofuatilia pambano la mwisho kabla ya hili hakuna kitu cha maana ambacho Salah alifanya uwanjani. Pambano lile la watani wa jadi kati ya Liverpool na Everton pale Goodson Park Salah alifanya nini uwanjani? Hakuna. Hata mwenzake ambaye aliamulia ugomvi wake na Klopp, Darwin Nunez hakuna kitu cha maana alichofanya. Haikushangaza kuona wote wakipigwa benchi na Klopp mechi hii dhidi ya Everton.
Salah aliamua kuweka hasira zake hadharani. Ingekuwa wakati ule mradi wao ukiwa umekolea sidhani kama angefanya hivi. Wachezaji ukasirika kuwekwa benchi, ukasirika kuingia baadae, ukasirika kutolewa lakini wengi wanajitahidi kuficha hasira. Misimu mitatu nyuma Salah angeficha hasira zake.
Kwa sasa hawezi kuficha hasira kwa sababu anajua kila kitu kimefika mwisho. Huwa inawatokea wachezaji. Roy Keane wakati akiwa anakaribia mwisho mwisho wa maisha yake ya soka Old Trafford aliwahi kwenda katika kituo cha Televisheni cha Manchester United na kuwapaka vilivyo wachezaji wa timu hiyo huku akidai baadhi yao hawakuwa na hadhi ya kuchezea timu hiyo.
Alijua alichokuwa anafanya. Alijua Sir Alex Ferguson angekasirika popote alipo katika kochi alilokuwa amekaa akitazama mahojiano hayo. Kweli alikasirika kiasi cha kupiga simu na kuamuru mahojiano hayo yasitishwe kwa haraka. Hata hivyo, Keane hakujali sana kwa sababu alikuwa katika siku za mwisho mwisho za maisha yake ya soka Old Trafford.
Kilichofuata ni mkataba wa Keane kusitishwa Old Trafford. Akajikuta akiangukia kucheza Celtic ya Uskochi. Timu ambayo alikuwa anaishabikia akiwa mtoto. Unapata shida kuamini yote haya yangetokea kama Keane angekuwa katika ubora wake. Unapata shida pia kuamini Sir Alex angeweza kuvunja mkataba wa Keane akiwa katika ubora wake.
Ni wazi Anfield inafanya sherehe baada ya mitihani. Kwa wale waliokuwa katika mradi mkubwa ambao sasa unakaribia kufika ukingoni ni wazi kila mtu ameanza kuwaza maisha nje ya Anfield. Hiki ndio chanzo cha ugomvi wa Bwana Klopp na mwanafunzi wake Salah.
Hata kwa upande wa Klopp kuna baadhi ya vitu ameanza kutohofia sana. Kwa mfano, angewezaje kumweka nje Salah katika mechi kama hii misimu miwili iliyopita. Mchezaji wa aina ya Salah ni wale wachezaji ambao unaamini anaweza kufanya lolote muda wowote hata kama hayupo katika fomu nzuri.
Usiamini katika misimu yote tangu awe bora pale Anfield hakuwahi kupoteza fomu yake. Ukweli ni, alipoteza lakini Klopp hakujali sana kwa sababu alikuwa ana matumaini muda wowote Salah angeweza kufanya kitu chochote uwanjani hata kama anapitia nyakati mbovu. Hata hivyo, Klopp anafahamu anaondoka na haoni kama ana muda wa kufikiria mahusiano yake yajayo na Salah.
Mwisho wa yote tunashuhudia mwisho wa zama zao. Zilikuwa zama za kusisimua Anfield. Walitengeneza timu tishio ambayo kwa sasa inamong’onyoka. Hata hivyo, asili ndivyo ilivyo. Mambo ufika mwisho.
Tumsubiri kocha ajaye. Ni wazi akina Salah hawatakuwa wachezaji na wakati huo Klopp atakuwa amekaa katika kochi akiitazama Liverpool akiwa nyumbani kwao Stuttgart.