Putin, Pezeshkian waahidi kuimarisha uhusiano

 

RAIS Vladimir Putin wa Urusi amefanya mazungumzo na mwenzake wa Iran, Masoud Pezekshian, nchini Turkemistan, ukiwa ni mkutano wa kwanza baina yao.

Kwenye mkutano huo wa jana, viongozi hao walisifu kuimarika kwa uhusiano wa kiuchumi katika mataifa yao na mitazamo yao inayofanana kwenye siasa za dunia.

Putin, ambaye nchi yake itakuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele wa mataifa ya BRICS mjini Kazan, wiki mbili zijazo, amemwalika Pezeshkian, kufanya ziara rasmi ya kiserikali nchini Urusi, mwaliko ambao umekubaliwa.

Taarifa ya kukutana kwa viongozi hao, imeripotiwa na Shirika la habari la Iran (IRNA), ambalo limemkariri Pezeshkian akisema kuwa uhusiano wa kiuchumi, kitamaduni na mawasiliano, unazidi kuimarika kati ya Moscow na Tehran.

Taarifa ya kuimarika kwao inakuja wakati ambao mataifa ya Magharibi yanakosoa uhusiano huo, kwa kile kinachodaiwa kuwa Moscow na Tehran, ni adui wa Magharibi.

Mkutano wa BRICS umepangwa kufanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe Oktoba 22 hadi 24, mwaka huu.
BRICS ni muungano wa nchi ya Brazili, Urusi, India, China na Afrika Kusini, zikitajwa kama nchi zenye kipato cha kati ambazo uchumi wake unakua kwa kasi.

Zinatabiriwa kuwa nchi zitakazoongoza kwa uchumi duniani ifikapo mwaka 2050.

About The Author

Related Posts