Aliyekuwa Waziri wa Fedha Mustafa Mkulo afariki dunia

Dar es Salaam. Aliyekuwa Waziri wa Fedha na Mbunge wa Kilosa, Mustafa Mkulo amefariki dunia jana Mei 3, 2024 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alipokuwa akipatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa taarifa ya kutangaza kifo chake iliyotolewa na familia yake, msiba upo nyumbani kwa marehemu Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Maziko yake yanatarajiwa kufanyika nyumbani kwake Kilosa mkoani Morogoro, kesho Jumapili ya Mei 5, 2024 saa nne asubuhi.

Mkulo alikuwa mbunge wa Kilosa kwa miaka 10 hadi mwaka 2015 kabla ya kuacha kugombea kwa kile alichokidai anaruhusu wengine kuchangia mawazo yao katika kuliletea maendeleo Jimbo la Kilosa.

Alipokoma ubunge wake, nafasi yake ilichukuliwa na Mbaraka Bawaziri.

Wakati akiwa mbunge, alipata bahati ya kuchaguliwa kuwa Waziri wa Fedha katika Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Serikali ya Jakaya Kikwete kati ya mwaka 2007 na 2012.

Hata hivyo, Mei 2012, Mkulo alikuwa miongoni mwa mawaziri sita waliotemwa katika Baraza la Mawaziri na kila mmoja aliachwa kwa sababu zake.

Mawaziri hao waliotemwa walikuwa wakiziongoza wizara nyeti zinazosimamia rasilimali za nchi na huduma za afya na uchukuzi.

Wengine waliong’olewa ni William Ngeleja (Nishati na Madini), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Omari Nundu (chukuzi), Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara) Dk Haji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii).

Pia, panga hilo liliwakumba waliokuwa Naibu Mawaziri, Dk Lucy Nkya (Afya na Ustawi wa Jamii) na Dk Athuman Mfutakamba (Uchukuzi).

Akizungumzia namna anavyomfahamu Mkulo, mbunge wa zamani wa majimbo ya Kigoma Mjini na Kaskazini, Zitto Kabwe amesema anakumbuka wakati Mkulo anakuwa Waziri wa Fedha, ndiyo kilikuwa kipindi kigumu cha sakata la Escrow.

Sakata hilo lilihusishwa uchotaji wa Sh320 bilioni kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Akaunti hiyo ilianzishwa kumaliza mgogoro wa malipo kati ya IPTL na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

“Tulikwazana na Mkulo kwa hoja sio kwa ubaya kuhusu mgogoro wa Shirika la Consolidated Holdings, lakini pia wakati wa marehemu ndiyo kulikuwa kashikashi ya sakata la Epa (Akaunti ya Madeni ya Nje),” anasema Zitto ambaye alikuwa waziri kivuli wa fedha na uchumi wakati huo.

Zitto alikumbushia namna walivyohakikisha usimamizi ofisi ya deni la Taifa linarejeshwa wizara ya fedha badala ya kubaki katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wakati Mkulo akiwa waziri wa sekta hiyo.

“Mara mwisho nilikutana na Mzee Mkulo katika msiba wa Membe (Bernard-aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje) Mungu ailaze pema peponi roho yake,” amesema Zitto.

Hadi umauti unamkuta, Mkulo amewahi kufanya kazi katika ofisi tofauti ndani ya Serikali ya Tanzania ikiwamo Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Ofisi ya Msajili wa hazina na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Related Posts