Waziri Mkuu awataka Vijana kujiepusha na matumizi mabaya ya mitandao ya kidijitali

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewahimiza vijana wa Tanzania kuepuka matumizi mabaya ya mitandao ya kidijitali ambayo yanaweza kuleta madhara kwa jamii kwa kuhamasisha chuki, udhalilishaji, na utengano. Majaliwa alisisitiza kuwa hali hiyo haina maslahi kwa Taifa, kwani Tanzania inajivunia amani, mshikamano, na upendo kati ya wananchi wake.

Akizungumza jijini Mwanza wakati akifungua maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yenye kaulimbiu, “Vijana na Matumizi ya Fursa za Kidijitali kwa Maendeleo Endelevu,” Waziri Mkuu alisema, “Kuaibishana, kutukanana, na kudhalilishana kupitia mitandao haina faida yoyote. Pamoja na sheria zilizopo za kudhibiti hali hii, ni muhimu kutumia mitandao ya kidijitali kwa njia zinazojenga mshikamano na kuchangia maendeleo ya jamii.”

Majaliwa pia aliwataka vijana kuchangamkia fursa za kidijitali na kutumia teknolojia kama nyenzo ya kujikwamua kiuchumi kwa ubunifu katika masuala ya kiteknolojia.

“Vijana changamkieni fursa zinazotokana na teknolojia ya kidijitali. Mnaweza kujipatia kipato, kukuza uchumi wa Taifa, na kutafuta masoko,” alisema Majaliwa.

Aidha, Waziri Mkuu aliwaasa viongozi wanaohusika na masuala ya vijana, akiwemo Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), kuendelea kuwasaidia vijana ili wapate msaada wa kujikwamua kiuchumi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwan Kikwete, aliongeza kuwa vijana ni nguzo ya mabadiliko nchini, hivyo hawawezi kuepuka matumizi ya mitandao ya kidijitali.

“Tutumie mifumo ya kidijitali vizuri, tusiipeleke kwenye matumizi yanayoeneza chuki na mpasuko mkubwa. Tuendelee kutumia mifumo hii ili itusaidie kufikia malengo yetu kama Taifa,” alisema Kikwete.

Maadhimisho haya yana lengo la kuwahakikishia vijana kuwa serikali inaendelea kuwawezesha kwa kutoa fursa mbalimbali ili wapate nafasi ya kujitambua na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Related Posts