UWEKEZAJI KATIKA MALEZI NA MAKUZI YA WATOTO NI MSINGI WA TAIFA IMARA- NAIBU WAZIRI MWANAIDI

Na WMJJWM, Dar ES Salaam

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis ametoa wito kwa jamii hususani kina Mama kuwekeza katika malezi na makuzi ya awali kwa watoto ili kupata Jamii yenye afya ya mwili, akili na kiroho.

Mhe. Mwanaidi ameyabainisha hayo katika hafla ya Jubilee ya kina Mama yenye lengo la kusherekea na kutoa elimu kwa Wanawake ili kuwasaidia kuboresha malezi na makuzi ya Watoto iliyofanyika Oktoba 12, 2024, Mkoani Dar Es Salaam.

Naibu Waziri Mwanaidi amefafanua kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua na kuheshimu mchango unaotolewa na sekta binafsi katika usimamizi na utekelezaji wa afua mbalimbali hususani utoaji wa elimu kwa umma kuhusu malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.

“Nimefarijika kuona ushirikiano mzuri uliopo baina ya Kampuni ya Jubilee Health Insurance na Wananchi ambao unaishi kwa vitendo kwani tumeona kuna ushirikishaji jamii katika utoaji wa elimu ya Malezi na Makuzi ya Mtoto ambayo inatolewa kwa Wanawake wanachama na wasio wanachama” amesema Naibu Waziri Mwanaidi

Aidha Mhe. Mwanaidi amewakumbusha wanawake kuwa Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum inaendelea kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Program ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi hususani Wanawake ili waweze kufikia malengo kikamilifu na kwa wakati kwa lengo la kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia.

“Napenda mtambue kuwa milango ya Wizara ipo wazi, hivyo nitumie fursa hii kuwakaribisha Wizarani ili tupange, tuandae na kutekeleza afua mbalimbali kwa pamoja hivyo yatupasa kuimarisha ushirikiano uliopo kwa lengo la kuwawezesha Wanawake kupata maarifa na rasilimali zitakazowawezesha kulea Watoto kwa maslahi ya familia na taifa kwa ujumla kwani tunaamini Familia Bora ndiyo msingi wa kuwa na Taifa Imara” amesisitiza Naibu Waziri Mwanaidi.

Kwa upande wake Dkt Angela Nanyaro kutoka Jubilee insurance ameishukuru Serikali kwa kuweka Uratibu mzuri kwa wadau malezi na makuzi ya watoto kwa kuunga mkono juhudi zinazowekwa na wadau hao ili kupata Jamii inayojitambua na imara .

“Serikali imeshawekeza vya kutosha katika malezi na makuzi hivyo kilichobaki ni sisi wanawake kuhakikisha tunawekeza kwa watoto wetu kuanzia umri wa 0-8 kwani huo ndiyo umri ambao watoto hujifunza mambo mengi na yanaoishi kwenye ubongo wao kwa maisha yao yote” amesema Dkt. Angela.

Vilevile Mtaalam wa Malezi na Makuzi Irene Fugale amewakumbusha wazazi kujenga uhusiano wa karibu na watoto wao ili kuweza kuwasaidia watoto wao kuwaamini na kuweza kuwaeleza pale wanapokumbwa na changamoto hususani changamoto ya ukatili kutoka kwa jamii.

Related Posts