KADA WA CHADEMA AFUNGIWA MIEZi 6 LESENI YA UDEREVA


NA DENIS MLOWE,IRINGA

JESHI la polisi kitengo cha usalama barabarani mkoa Iringa kimemfungia leseni ya Udereva kwa kipindi cha miezi 6 kuanzia tarehe 7 mwezi 10 mwaka huu Kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Vitus Nkuna (29) Mnyambo, mjasiriamali, mkazi wa Mwangata Manispaa Iringa.

Akizungumza mbele ya wanahabari Kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa SACP Allan Bukumbi alisema kuwa licha ya kufungiwa leseni Nkuna amelipa faini kwa kosa la kuendesha gari akiwa amelewa na kusababisha ajali akiwa anaendesha gari yenye namba za usajili T 797 DYC aina ya volkswagen na kugonga gari yenye namba T 975 EDC aina ya Toyota probox tarehe 30/9 mwaka huu.

Alisema kuwa awali Nkuna ambaye ni mwanachama wa Chadema alikamatwa kwa kosa la kusababisha ajali na kusambaza taarifa za uwongo kwenye mtandao wa X kuwa ameshambuliwa na watu wasiojulikana akiwa barabarani mkoani Iringa baada ya mapambano na kupelekwa kituo cha polisi Iringa.

Alisema kwamba kesi ya kusambaza taarifa za uwongo bado iko mahakamani na ikitolewa hukumu jamii itapewa taarifa kupitia vyombo vya habari.

Katika tukio jingine Musa Omary mkazi wa Dodoma amefungiwa leseni kuanzia tarehe 3 Septemba hadi shauri lake likapokwisha mahakamani kwa kosa la kusababisha ajali akiwa anaendesha gari yenye namba za usajili DFPA 9917 aina ya Toyota Land Cruiser na kumgonga mtembea kwa miguu aitwaye Martine Mgaya eneo la Ifunda na kumsababishia kifo.

Bukumbi ameongeza kuwa mtu mwingine aliyefungiwa leseni ni Cleophas Mahali mkazi wa Uyole Mbeya amefungiwa leseni kwa muda wa miezi 6 kuanzia tarehe 10 Septemba mwaka huu kwa kosa la kulipita gari lilokuwa mbele yake kwenye kona kali eneo la mlima Kitonga bila kuchukua tahadhali akiwa anaendesha gari yenye namba za usajili T 710 DPS basi aina ya Yutong Mali ya kampuni ya Mbeya City.

Wakati huo jeshi la polisi mkoa wa iringa kutokana na doria na misako inayoendelea kufanyika wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 46 kwa makosa ya wizi wa mali mbalimbali ikiwemo pikipiki 23 aina tofauti na kati ya hizo 16 hazina namba za usajili, runinga 9 zenye ukubwa tofauti, simu nne aina ya Tecno na Samsung na Godoro moja (5×6).

Ameongeza kuwa vitu vingine vilivyokamatwa ni mtungi mdogo wa gesi aina ya ORYX , Madumu 16 ya Lita 20 kila moja, kati ya hayo, madumu 10, yakiwa na mafuta aina ya dizeli , Redio tatu aina tofauti na fulana na kofia mbili za Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Kamanda Bukumbi ametoa wito kwa wananchi kufika jeshi la polisi kutambua Mali mbalimbali ambazo wamefanikiwa kuzikamata kutokana na doria wanazofanya mara kwa mara.

 

Related Posts