RAIS SAMIA ASISITIZA VIJANA KULINDA AFYA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,akizungumza leo Oktoba 14, 2024, katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kwenye hitimisho la Wiki ya Vijana, kumbukizi ya miaka 25 ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, pamoja na Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2024.

Na Adelina Johnbosco, Mwanza

‘’Vijana tambueni kuwa, dunia na nchi yetu kuna changamoto kadhaa dhidi yenu ikiwemo; madawa ya kulevya na magonjwa, hivyo kuweni makini jiepushe nayo, jikinge na maradhi hasa Ukimwi, fanyeni mazoezi na michezo pamoja na kula lishe bora ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza’’

Hiyo ni rai ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwataka vijana nchini kote kuzilinda na kutunza afya zao dhidi ya magonjwa kwani wao ni tunu na kundi linalotegemewa katika maendeleo ya Taifa.

Mhe.Rais ameyasema hayo leo Oktoba 14, 2024, katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kwenye hitimisho la Wiki ya Vijana, kumbukizi ya miaka 25 ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, pamoja na Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2024.

Aidha, Rais Samia amewapongeza vijana sita walioongoza mbio za Mwenge wa Uhuru nchi nzima, ambapo amesema wamekuwa kielelezo cha mojawapo ya maudhui ya Mwenge huo ya kuhamasisha umoja, upendo, mshikamano, amani na kupinga matendo maovu nchini.

‘’Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alikuwa na falsafa ya kupenda usawa, alichukia ufisadi, rushwa, chuki na dharau kwa binadamu. Hili ndilo chimbuko la Mwenge wa Uhuru nchini kwetu. Maono na fikra zake zimeendelea kuishi hata baada ya kifo chake, aliweza kutuunganisha na kudumisha amani, tukaongea lugha moja kwa upendo tukiwa makabila zaidi ya 120’’ ameongeza Rais Samia

Mhe. Rais Samia ametanabahisha kuwa, anatambua changamoto zinazowakabili vijana nchini na kuwahakikishia juu ya uwepo wa mikakati madhubuti ambayo Serikali inaendelea kuweka ili kuhakikisha zinaondolewa kwa maslahi ya vijana wenyewe na taifa, huku akisema Serikali sikivu imepokea maoni, ushauri na mapendekezo kutoka kwa wakimbiza Mwenge na kuahidi kuyafanyia kazi.

Related Posts