Wakati Iran ilipovurumisha makombora 180 ya masafa marefu kuelekea Israel wiki moja iliyopita na kusababisha uharibifu mdogo na watu kujeruhiwa, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, alionya kwamba Tehran ilifanya kosa kubwa huku akiahidi kulipiza kisasi.
Shambulio la kwanza la Iran dhidi ya Israel mwezi Aprili lililojumuisha droni 300 na makombora lilijibiwa kwa hatua za wastani. Lakini maafisa wa Israel mara hii wameapa kulipiza kisasi kwa nguvu kubwa na hivyo kuchochea uvumi kwamba Israel inaweza kuilenga miundombinu ya mafuta, kijeshi na nyuklia ya Iran.
Soma pia: Marekani kupeleka askari wake Israel
Netanyahu anakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa baadhi ya maafisa wakuu wa Israel, akiwemo Waziri Mkuu wa zamani, Yair Lapid, kushambulia maeneo nyeti ya Iran, huku Rais wa Marekani Joe Biden akitoa wito wa kujizuia, huku akisema mnamo Oktoba 4 kuwa ikiwa angelikuwa katika nafasi ya Israel angelivishambulia miundombinu ya mafuta ya Iran.
Bei ya mafuta yapanda kutokana na hatari ya mizozo ya kimataifa
Tangu kutokea mashambulizi ya hivi karibuni ya Iran, bei ya mafuta imepanda maradufu. Mafuta ghafi yamepanda kwa asilimia 17 katika wiki moja hadi kufikia dola 81.16, ingawa bei zimepungua tena baada ya wanamgambo wa Hezbollah wanaoungwa mkono na Iran kuashiria utayari wa kusitisha mapigano katika mzozo wake na Israel katika eneo la mpaka na Lebanon.
Iwapo Israel itashambulia na kuharibu miundombinu muhimu ya mafuta ya Iran, hilo linaweza kuondoa upatikanaji wa karibu mapipa milioni 2 kwa siku kwenye soko la kimataifa la mafuta, na hivyo kusababisha baadhi ya wafanyabiashara kuhofia kwamba bei ya mafuta inaweza tena kupanda. Kwa mara ya mwisho, bei ya mafuta ilifikia dola 100 kwa pipa, muda mfupi tu baada ya Urusi kuanzisha uvamizi wake kamili nchini Ukraine mnamo Februari mwaka 2022.
Wengine wanahofia bei ya mafuta kufikia dola 200 kwa pipa
Bjarne Schiedrop, mchambuzi mkuu katika benki ya Sweden (SEB), aliliambia wiki iliyopita shirika la utangazaji la Marekani CNBC kuwa ikiwa Israel itaangamiza vituo vya mafuta nchini Iran, basi bei ya mafuta inaweza haraka kufikia dola 200 au zaidi kwa pipa moja.
Soma pia: Ayatullah Ali Khamenei atetea kuishambulia Israel
Iran ambayo ni moja ya wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani, inakabiliwa na vikwazo vikali vya kimataifa katika suala zima la uuzaji wa nje wa mafuta kutokana na mzozo wa muda mrefu na nchi za Magharibi juu ya malengo ya Tehran ya kuanzisha silaha za nyuklia.
Lakini licha ya hayo, mauzo ya mafuta ya Iran yalifikia kiwango cha juu katika kipindi cha miaka mitano kwa kuuza mapipa milioni 1.7 mwezi Mei, hii ikiwa ni kulingana na kampuni ya Vortexa ambayo ni ya ufuatiliaji wa masuala ya nishati.
Takriban asilimia 90 ya mafuta ya Iran yanauzwa kinyume cha sheria nchini China, kwa kutumia karibu meli 400 za Iran ambazo husafirisha kimagendo na kutumia mbinu mbalimbali ili kukiuka vikwazo hivyo.
Carole Nakhle, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la ushauri la Crystol Energy lenye makao yake mjini London- Uingereza, ameiambia DW kuwa uchumi wa Iran unategemea mno mapato inayoyapata kutokana na mauzo yake ya mafuta na kwamba usumbufu wowote kwenye mapato hayo utakuwa na athari kubwa kwa uchumi wa taifa hilo.
Lakini wachambuzi wengine wanasema kuna uwezekano mkubwa Israel ikashambulia miundombinu ya kijeshi na kuzilenga zaidi taasisi za serikali ya mjini Tehran.