Katika taarifa, Khan amesema ghasia za hivi karibuni jimboni Kivu Kaskazini zinahusishwa na matukio ya vurugu na uhasama ambayo yamekumba eneo hilo tangu katikati mwa mwaka 2002. Kutokana na hilo, tuhuma za hivi karibuni zaidi zinaangukia kwenye uchunguzi unaoendelea.
Khan asema uchunguzi Kivu Kaskazini hautakuwa wa upendeleo
Khan amesema uchunguzi wake huko Kivu Kaskazini hautahusisha vyama ama wanachama wa makundi maalumu lakini badala yake, ofisi yake itachunguza kiujumla, kwa njia huru, na bila upendeleo wahusika wote wanaodaiwa kufanya uhalifu ndani ya mamlaka ya mahakama hiyo.
Uamuzi huo pia unafuatia rufaa ya pili kutoka kwa serikali ya Kongo mnamo Mei 2023, ambayo iliomba uchunguzi katika kile ambacho nchi hiyo iliutaja kuwa uporaji wa kimfumo wa raslimali zake asili masharikimwa Kongo kutoka kwa Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) na kundi la waasi la M23.
Awali waasi watatu walitiwa hatiani na Mahakama ya ICC
Awali, mahakama hiyo ya ICC iliwatia hatiani waasi watatu kwa uhalifu katika mkoa wa Ituri, kaskazini mwa Kongo ikiwa ni pamoja na mbabe maarufu wa vita Bosco Ntaganda, anayejulikana kama “The Terminator” ambaye alipatikana na hatia ya uhalifu ikiwa ni pamoja na mauaji, ubakaji na utumwa wa ngono.