Taarifa kwamba Israel itasikiliza maoni ya Marekani lakini wakati wote itachukua hatua kwa kuzingatia maslahi yake ya kitaifa imetolewa ili kujibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu ripoti iliyochapishwa kwenye jarida la Washington Post juu ya maafisa ambao hawakutajwa majina waliosema kuwa Netanyahu alimwambia Rais wa Maredkani Joe Biden kwamba Israel inapanga kuvishambulia vituo vya kijeshi vya Iran na sio maeneo ya mafuta au nyuklia.
Soma Pia: Israel yashambulia makao makuu ya UN Lebanon
Jarida hilo limeripoti kwamba Netanyahu anatayarisha mashambulizi ya kulipiza kisasi, kujibu shambulio la makombora dhidi ya Israel lililofanywa na Iran wiki mbili zilizopita.
Kuna hofu kwamba Mashariki ya Kati iko kwenye njia ya kutumbukia kwenye vita kamili vya kikanda kutokana na mvutano unaoongezeka kati ya Israel na Iran. Aidha, Israel imeifahamisha Marekani kwamba itamaliza operesheni yake dhidi ya wanamgambo wa Hezbollah wanaoungwa mkono na Iran nchini Lebanon katika wiki zijazo.
Emiri wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani amesema ni muhimu kuimaliza mivutano na mapigano huko nchini Lebanon. Ametoa wito wa kukomeshwa mapigano huko Lebanon na tukutekelezwa maazimio ya kimataifa likiwemo azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la mwaka 2006.
Vyombo vya habari rasmi vya Lebanon vmeiripoti kwamba jeshi la Israel hii leo Jumanne limeanzisha mashambulizi upande wa mashariki mwa Lebanon, na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa kutolihurumia kundi la wanamgambo wa Hezbollah.
Soma Zaidi: EU kupeleka kitita cha msaada wa kiutu Lebanon
Katika Ukanda wa Gaza wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas imesema hadi hii leo takriban watu 42,344 wameuawa katika vita kati ya Israel na wanamgambo wa Palestina.
Idadi hiyo inajumuisha vifo 55 katika muda wa saa 24 zilizopita, kwa mujibu wa wizara hiyo, watu 99,013 wamejeruhiwa katika Ukanda wa Gaza tangu vita vilipoanza baada ya wapiganaji wa Hamas walipoishambulia Israel mnamo Oktoba 7, mwaka jana.
Vyanzo: AFP/DPA/