Waziri atoa maelekezo FITI – Mtanzania

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dk. Pindi Chana amekielekeza Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi (FITI) kujitangaza ili kupata soko la kuuza bidhaa za misitu zinazozalishwa na chuo hicho.

Ametoa kauli hiyo leo Oktoba 15,2024 alipozungumza na uongozi wa chuo hicho wakati wa ziara ya kikazi katika chuoni hapo Moshi, mkoani Kilimanjaro.

“Tuendelee na mashirikiano kati yetu na vyuo vingine vilivyopo hapa nchini na tujitangaze ili bidhaa zinazotokana na mazao ya misitu, ziuzike hasa kwenye taasisi za Serikali,” amesema Dk. Chana.

Aidha, ameielekeza Menejimenti hiyo kuhakikisha mapato ya chuo yanaongezeka ili kiweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Pia ameelekeza chuo hicho kutoa mafunzo ya utengenezaji mizinga ya nyuki kwa wananchi ili waweze kufuga asali na hatimaye kujikwamua kiuchumi.

Naye, Mkuu wa Chuo hicho, Dk Zacharia Lupala amesema chuo kimejikita katika kutoa maarifa, ujuzi na huduma ya ugani katika matumizi endelevu ya rasilimali za misitu na hifadhi za mazingira.

Related Posts