Kiongozi wa chama cha Umkhonto we Sizwe nchini Afrika Kusini, Dk. John Hlophe, amelezea kuwa hatua ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma jimboni Limpopo kutomfungulia mashtaka Rais Cyril Ramaphosa ni aibu kubwa kwa nchi. Dk. Hlophe anasisitiza kuwa Rais Ramaphosa ana kesi ya kujibu, ikiwa ni pamoja na tuhuma za kukwepa kulipa kodi.
Chama cha Wapigania Uhuru wa Kiuchumi (EFF), chini ya mwenyekiti wake Julius Malema, kimesema kina ushahidi wa kutosha kumfungulia mashtaka Rais Ramaphosa na kimepanga kuwasilisha hoja bungeni ili wabunge wapige kura ya kutokuwa na imani na Rais.
Hii ni katika mazingira ambapo mjadala unaendelea kuzua hisia miongoni mwa wananchi, huku wengi wakihoji ni kwanini mkurugenzi wa mashtaka ya umma aliamua kumfutia kesi Rais.
Soma pia: Ramaphosa akabiliwa tena na mchakato wa kumuondowa
Wakati huo huo, maswali yanaibuka kuhusu kitita cha dola milioni nne taslimu kilichopatikana kimefichwa chini ya makochi badala ya kupelekwa benki. Sakata hili linaweza kuwa na athari kubwa kwa utawala wa Rais Ramaphosa, ambaye anakabiliwa na kashfa kadhaa zinazohusiana na ufisadi.
Julius Malema: “Kesi ya wizi na utakatishaji fedha bado inaanza.”
Julius Malema amesema kuwa kesi ya wizi na utakatishaji fedha iliyofutwa na mwendesha mashitaka wa jimbo la Limpopo ni mwanzo tu. Anabainisha kuwa, “Siku ya Ramaphosa mahakamani inakuja pamoja na mamlaka huru ya mwendesha mashitaka. Bunge linaweza kupita na Ramaphosa akashtakiwa kwa sababu unaweza kupigiwa kura ya kutokuwa na imani hata ukiwa umetoka madarakani.”
Mwaka 2020, mkuu wa zamani wa kitengo cha ujasusi alileta malalamiko ya jinai dhidi ya Ramaphosa kuhusu wizi wa dola milioni nne taslimu katika shamba lake la Phala Phala. Uchunguzi wa kitengo maalum cha polisi ulishindwa kumfungulia mashtaka yeyote, hatua iliyosababisha hasira miongoni mwa wanasiasa na umma.
Soma pia: ANC, DA wakubaliana kuunda serikali Afrika Kusini
Mukhali Ivy Thenga, mwendesha mashitaka wa Limpopo, alikiri kuwa ni muhimu Rais ashtakiwe kutokana na ukweli kwamba fedha hizo hazikuwekwa wazi kwa umma. “Rais ana hatia ya kukwepa kulipa kodi,” alisema.
Zimwi la rushwa lawandama marais Afrika Kusini
Ikumbukwe kuwa Rais wa awamu ya pili baada ya utawala wa ubaguzi wa rangi, Thabo Mbeki, aliondolewa madarakani baada ya chama chake kumtaka aachie ngazi, na mrithi wake, Jacob Zuma, naye alikumbana na kashfa za ufisadi.
Mchambuzi wa siasa Mudeba Fisto ametoa wito wa kufuatilia sakata hili kwa ukaribu. “Ni muhimu kulifuatilia, kwani linaweza kuwa na athari kwa rais mwingine atakayefuata,” alisema.
Kwa upande mwingine, Mahakama ya Katiba tayari imekubali kusikiliza maombi yaliyowasilishwa na EFF na chama cha ATM, ambapo vyama hivyo vinaitaka mahakama ichunguze hatua za bunge kuhusu kesi ya kumtimua madarakani Rais Ramaphosa.