Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, ameithibitishia Jumuiya ya Kimataifa kuwa masuala ya demokrasia na haki za binadamu yataendelea kuimarika zaidi nchini Tanzania chini ya uongozi wa Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Balozi Nchimbi aliyasema hayo alipokutana na Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Mhe. Dr. Mehmet Güllüoğlu, Balozi wa Morocco, Mhe. Zacharia El Goumir, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Sera na Tathmini wa Taasisi ya Misaada ya Marekani (MCC), kwa nyakati tofauti, leo Jumanne, tarehe 15 Oktoba 2024.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar es Salaam, Balozi Nchimbi amesema katika kipindi cha uongozi wa serikali ya awamu ya sita, hatua kubwa imefikiwa katika kuimarisha demokrasia, utawala bora, uchumi na haki za kiraia.
Mazungumzo hayo ya Balozi Nchimbi na mabalozi wa nchi hizo, pamoja na taasisi ya MCC, yalilenga kuboresha uhusiano katika nyanja mbalimbali, zikiwemo siasa, kilimo, teknolojia, elimu, na michezo, kwa lengo la kuleta maendeleo ya pamoja kwa wananchi wa pande zote.
Katika kikao chake na Balozi wa Uturuki Mhe. Dkt. Güllüoğlu, Balozi Nchimbi alisisitiza kuwa uhusiano wa Tanzania na Uturuki ni wa kimkakati, huku akitaja ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kuwa ni mfano mmojawapo wa mafanikio ya ushirikiano huo.
Kwa upande wake, Mhe. Dr. Güllüoğlu alikubaliana na Balozi Nchimbi na akathibitisha kuwa Uturuki itaendelea kushirikiana na Tanzania katika miradi ya maendeleo, zikiwemo sekta za teknolojia, elimu na biashara ya mazao ya kilimo.
Katika mazungumzo yake na Balozi wa Morocco, Balozi Nchimbi aliishukuru nchi hiyo kwa mchango wake katika sekta ya elimu na michezo na kuipongeza kwa msaada wao wa ujenzi wa msikiti mkubwa kuliko yote Afrika Mashariki, uliojengwa eneo la Kinondoni jijiji Dar es Salaam.
Balozi Nchimbi alibainisha kuwa ushirikiano wa Tanzania na Morocco una manufaa makubwa kwa pande zote mbili, hasa katika kukuza elimu, michezo, na masuala ya usalama ndani ya Afrika.
Kwa upande wake Balozi wa Morocco Mhe. Goumir alithibitisha kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania, huku akieleza dhamira ya Morocco katika kusaidia maendeleo ya kitaaluma na michezo nchini Tanzania.
Aidha, mazungumzo ya Balozi Nchimbi na ujumbe wa MCC, uliongozwa na Mhe. Dan Barnes, yalijikita katika maeneo ya siasa, miradi ya maendeleo na utawala bora.
Balozi Nchimbi alisisitiza kuwa Serikali ya CCM, chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia, inaendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuboresha hali ya demokrasia na haki za binadamu nchini.
Balozi Nchimbi alisisitiza kuwa maendeleo haya ni sehemu ya dira ya serikali ya kuhakikisha kuwa haki za raia na utawala bora vinadumishwa, huku Tanzania ikiendelea kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika na dunia kwa ujumla.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi akizungumza na Balozi wa Morocco nchini Tanzania, Mhe. Zacharia El Goumir , leo tarehe 15 Oktoba 2024, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar Es Salaam.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Sera na Tathmini wa Taasisi ya Misaada ya Marekani (MCC), leo tarehe 15 Oktoba 2024, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar Es Salaam.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi akizungumza na Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Mhe. Dkt. Mehmet Gulluoglu , leo tarehe 15 oktoba 2024, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar Es Salaam.