Waziri wa zamani wa Oman Dkt. Mohammed Rumhy apewa ubalozi wa kukuza uwekezaji Zanzibar

Katika hatua muhimu ya kuvutia uwekezaji kutoka Oman kuja Zanzibar, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imemteua Dkt. Mohammed Hamed Saif Al Rumhy kuwa mwakilishi wa kukuza fursa za uwekezaji, hususan katika sekta ya nishati

Uteuzi huo umefanywa na Shariff Ali Shariff, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais kwa Masuala ya Kazi, Uchumi na Uwekezaji.

Dkt. Rumhy, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini wa Oman, ana uzoefu mkubwa na mtandao mpana wa uhusiano wa kimataifa. Uteuzi huu unalenga kuimarisha mahusiano ya kihistoria na kimkakati kati ya Zanzibar na Oman, na kuongeza juhudi za kuvutia wawekezaji kwenye visiwa vya Zanzibar.

Katika nafasi yake mpya, Dkt. Rumhy atawajibika kuwasiliana na wawekezaji na wadau kutoka Nchi za Ghuba (GCC) na maeneo mengine duniani. Kwa kutumia maarifa na uhusiano wake, atakuwa na jukumu la kuonyesha fursa za kipekee za uwekezaji zinazopatikana Zanzibar, akisisitiza faida za kimkakati za kuwekeza katika eneo hili.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ina imani kwamba ushirikiano wa Dkt. Rumhy utaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kufikia malengo ya maendeleo ya Zanzibar. Utaalamu wake unatarajiwa kuimarisha ushirikiano ambao ni muhimu kwa ukuaji wa kiuchumi wa visiwa vya Zanzibar, na kuimarisha uhusiano wa kimkakati kati ya Zanzibar na Oman.

Mheshimiwa Waziri Shariff Ali. Shariff amewaomba wadau wote kutoa ushirikiano na msaada wao kwa Dkt. Rumhy katika juhudi hii muhimu, ambayo inatarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi wa kiuchumi wa Zanzibar.

Uteuzi huu ni sehemu ya jitihada za ufuatiliaji wa ziara ya Kitaifa ya Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, aliofanya mwishoni mwa mwaka 2022 na kufuatiwa na ziara ya Dkt. Rumhy visiwani Zanzibar ambapo alikutana na Dkt. Mwinyi na kumuahidi kwamba baada ya kustaafu kwake nchini Oman angependa kutumia ujuzi na uzowefu wake kuisaidia Zanzibar.

Ikumbukwe kwamba Dkt. Mohammed Al Rumhy alizaliwa na kuanzia elimu yake kisiwani Pemba na badae kuelekea Oman akiwa na umri wa miaka 14. Rumhy ni moja ya viongozi wanaoheshimika sana nchini Oman na alihudumu katika Wizara ya Nishati na Madini kwa miaka 24 mfululizo hadi ilipostaafu miaka michache uliopita. Mwaka 2017 aliongoza ujumbe ulioleta salaam za amani kutoka kwa Al Marhoom Mfalme Qaboos.

Ujumbe wake ulisafiri kuja Zanzibar, Dar es Salaam na badae Mombasa kwa kutumia Meli ya Fulk Al Salaam iliotia nanga bandari ya Malindi.

Related Posts