Mwanza. Hospitali ya Rufaa Kanda ya Bugando (BMC) inatarajia kukusanya zaidi ya Sh1 bilioni kwa ajili ya kuwezesha matibabu ya saratani kwa watoto 500.
Akizungumza leo Mei 4, 2024 wakati wa uzinduzi wa mbio za Bugando Health Marathon 2024 zinazolenga kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwezesha matibabu hayo, Daktari bingwa mbobezi wa magonjwa ya saratani ya watoto, Heronima Kashaigili amesema mbali na kupata msaada wa fedha za matibabu kutoka serikalini na kwa wadau, hazitoshi kutokana na idadi kubwa ya watoto wenye saratani.
“Mwaka 2009 tulianza kuona watoto 50 na ufanisi wake kutibu ulikuwa chini ya asilimia 20 ina maana karibu asilimia 35 ya watoto walikuwa wanakufa lakini hadi kufikia mwaka 2023 tunaweza kuona watoto 300 na tumefikia zaidi ya asilimia 50 ya kuweza kutibu watoto hao,” amesema.
“Pamoja na jitihada Serikali na wadau mbalimbali kutoa fedha kwa ajili ya matibabu, hazitoshi bado tuna changamoto nyingi mfano kukosa wataalamu wa kutosha, uelewa mdogo wa watoto kuhusu saratani upo chini na wagonjwa kuja wakiwa wamechelewa,” amesema Dk Kashaigili.
Pia, Dk Kashaigili ametaja saratani ambazo zimekuwa zikiwasumbua watoto wengi wanaofika hospitalini hapo ni ya matezi, figo, jicho, damu, misuli, ubongo, mifupa na mishipa ya fahamu.
Mkuu wa Idara ya Saratani hospitalini hapo, Nestory Masalu amesema tangu mwaka 2009 idara hiyo ilipoanzishwa idadi ya wagonjwa wa saratani inazidi kuongezeka huku changamoto kubwa ikiwa ni ucheleweshwaji na ukosefu wa fedha za matibabu.
“Tangu mwaka 2009 tulivyoanza idara ya saratani tuliona wagonjwa 320 lakini mpaka Januari mwaka huu tumeona wagonjwa jumla ya wagonjwa 73,000 kwa sasa tuna wastani wa kuona wagonjwa wa saratani 1,500 kwa mwaka na kati yao wagonjwa 300 ni watoto wa chini ya miaka 12,” amesema Masalu.
“Kwa hiyo utaona tuna wagonjwa wengi watu wazima na wengine watoto, lakini wagonjwa watu wazima wengi wanafika wakiwa wamechelewa kufika katika huduma.
Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk Fabian Massaga amesema wameamua kuja na mbio hizo ambazo kilele chake kitakuwa Agosti 31, 2024 mahususi kwa kuchangisha fedha kwa ajili kutoa msamaha na kugharamia matibabu ya watoto wanaokutwa na saratani.
“Baada ya uwekezaji mkubwa wa Serikali katika hospitali yetu hasa katika eneo la matibabu ya saratani na kupelekea hospitali yetu kuwa kituo cha matibabu ya saratani kwa kanda ya ziwa tumeendelea kushuhudia ongezeko kubwa la wagonjwa wa saratani wakiwamo watoto hali iliyosababisha uongozi wa hospitali kuja na mbio hizi kwa mwaka huu ili zitumike kuhamasisha na kuchangia fedha za matibabu ya saratani kwa watoto wasio na uwezo,” amesema Dk Massaga.
“Pamoja na kuhamasisha mazoezi ya viungo, lengo la mbio hizi ni kukusanya Sh1 bilioni au zaidi kwa ajili ya kusaidia gharama za matibabu kwa watoto takribani 500 watakaougua saratani na kauli mbiu ni kimbia, changia watoto wenye saratani,” amesema Dk Massaga
Akizindua mbio hizo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda mbali na kuchangia Sh5 milioni ametoa wito kwa taasisi na wadau mbalimbali kuunga jitihada za hospitali hiyo kwa kujiandikisha kushiriki mbio hizo sambamba na kuchangia.
“Takwimu zinaonyesha kadri miaka inavyoongezeka na idadi ya watoto wenye saratani inazidi kuongezeka, naomba nitoe wito kwetu sote tuungane kwa pamoja kusaidia watoto wanaougua saratani ili watibiwe kwa manufaa ya Taifa letu,” amesema Mtanda.
Uzinduzi wa mbio hizo umefanyika katika hospitalini hapo leo Mei 4, 2024 na kilele chake kitakuwa Agosti 31, 2024.