SIMBA inatarajia kutua jijini Dar es Salaam leo alasiri, ikitokea Zanzibar ambako iliweka kambi ya siku tatu, kujiandaa na Kariakoo Dabi dhidi ya mtani wake Yanga, itakayopigwa kesho kuanzia saa 11:00 jioni, Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa klabu hiyo, zinasema hadi kufikia saa tisa alasiri, watakuwa wamefika mjini na wataweka kambi kwenye hoteli moja ya kihafari, iliyopo jijini Dar es Salaam kabla ya kwenda kwenye mechi kesho jioni.
Kiongozi huyo ambaye hakutaka jina lake liwekwe wazi, amesema wamekamilisha maandalizi yao na wanaamini mechi itakuwa na ushindani mkubwa hivyo wamejiandaa kwa kila kitu.
“Saa 10:00 jioni timu itakuwa imefika Dar es Salaam, moja kwa moja tutakwenda kwenye hoteli moja ya kifahari hapa mjini, hii imekuwa kawaida yetu tukiwa na mechi ngumu ama mechi za kimataifa tunakaa mjini,” amesema.
Akiulizwa kuhusu usafiri wanaotumia kutoka Zanzibar kuja Dar es Salaam alisema: “Hilo siyo muhimu kulijua, jambo la msingi ni kurudi na tuendelee na ratiba nyingine ya mechi.”
Mzunguko wa kwanza, Simba ikiwa mwenyeji wa mchezo ilipigwa mabao 5-1 na mtani wake Yanga kwenye uwanja huohuo.