Faida, hasara kwa wanandoa kuchunguzana

Utafiti uliofanywa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) ulibaini simu ni miongoni mwa sababu zinazochangia ndoa nyingi, hasa za vijana wa sasa kuvunjika.

Hapa yanahusishwa matumizi ya simu kwa ujumla wake na athari zake kwa wenza, swali linakuja je, kuna haja ya kufuatilia mawasiliano ya mwenza wako ili kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa?

Ni picha mbili tofauti, wengine wakiamini ni ulinzi kwa mke au mume kumchunguza mwenza wake, lakini upande mwingine wanasema ni fedheha na jambo linalochochea uhusiano kuingia shubiri, mengine hadi kuvunjika.

 Picha hiyo inaakisi namna ndoa ya Janeth John ilivyovunjika Machi, mwaka huu, baada ya mumewe kuamua kumchunguza kwa kuikagua simu yake ya mkononi.

 “Bomu nililokutana nalo, sikuamini kama ni mke wangu, simu ya Sh500,000 ilivunja ndoa yetu iliyodumu kwa miaka saba,” anasema Charles Edward kwa masikitiko.

 Anasema kipindi chote kuanzia cha uchumba hakuwahi kushika simu ya mkewe, hadi siku moja wakiwa na zaidi ya miaka sita kwenye ndoa ndipo alishawishika kufanya hivyo.

“Niliona nyendo zake zinabadilika, ikabidi nianze kumchunguza, njia rahisi kwangu ilikuwa ni kwa kupitia simu yake, nilikuja kugundua mke wangu ana mahusiano na rafiki yangu,” anasema.

 Hata hivyo, kisheria Charles alifanya kosa, kama mkewe angeamua kumshtaki, sheria ingechukua mkondo wake.

 Wakili kiongozi wa kampuni ya Uwakili ya Haki Kwanza, Alloyce Komba anasema Charles alifanya kosa la kuingilia faragha ya mkewe.

 “Kama mkewe angemshtaki kwenye sheria adhabu yake ingeangalia baada ya kuingilia faragha ya mkewe, tukio hilo lilisababisha madhara gani? Kama mligombana, mkaumizana au madhara mengine,” anasema Komba.

 Anasema, japo sheria hiyo ya haki ya faragha haijali aliyeingilia ni mume au mke, wapo wanandoa wengine wanailegeza kwa utashi na upendo wao na kuivunja wenyewe kwa kupendana kwao.

Miongoni mwa wanaoilegeza sheria hiyo ni Samia Juma na mumewe, Mustafa Musa, ambao wanasema tangu kwenye uchumba wao hawakuwekeana mipaka kwenye simu.

“Naichunguza simu ya Mustafa wakati wowote ule, wakati mwingine hata ikiita naipokea, password (neno la siri) yake naifahamu na yangu anaifahamu, hatuoni shida kuishi hivyo,” anasema.

 Anasema, maisha hayo wanayafurahia, hakuna usiri kwenye simu zao wakiamini imewasaidia kuwakinga na mawasiliano yasiyofaa.

 “Hii imetusaidia kuwa makini, nilimwambia Mustafa mapema kabisa hata kabla ya ndoa yetu kwamba, sitoacha kukagua simu yake, kama akiona kuna kitu ambacho nikikiona tutakwazana, basi nisikikute, tunaishi hivyo mwaka wa tatu sasa katika ndoa yetu,” anasema.

 Robert Steven naye anaeleza namna asivyo na mipaka kwenye simu ya mkewe, vivyo hivyo naye simu yake mkewe yupo huru nayo.

Ingawa ni tofauti kwa Elias Paulo ambaye anasema kwa mwanamume anayejielewa mwenye mapenzi ya dhati na mkewe hata kama atachepuka, bado atatimiza majukumu yake.

“Mkianza kuchunguzana, simu ya mwenzako unataka kujua inapigwa au anawasiliana na akina nani, hapo ndipo tatizo linapoanzia.

“Hakuna kitu kinakera kwenye mahusiano kama hicho, lakini pia kinasababisha kwa asilimia kubwa hata ndoa kuvunjika, si jambo linalofaa hata kidogo,” anasema.

Paulo anasema katika ndoa kikubwa cha kuzingatia ni kumpenda mwenzako, ujilinde na kujitunza na magonjwa.

 “Kuna wengine, akishaona burungutu (pesa) huwa hajali, anachokiangalia ni kuchepuka ili apate hizo pesa, bila kujali hata afya yake na ya mwenza wake, na ustawi wa familia yao,” anasema.

Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Daniel Sendoro anasema katika ndoa hakuna usiri, kila mmoja anapaswa kuwa huru kwa mwenzake.

“Ndoa ni makubaliano, hivyo hata maisha ya wanandoa yanategemeana na matokeo ya makubaliano.

 “Mnapoamua kuingia huko, kuna mambo mnakubaliana kabla, hata kwenye matumizi ya simu ni mambo ya faragha, mnapaswa mkubaliane kukaguana au kufuatiliana, japo mnapoingia kwenye ndoa hakuna siri kati yenu,” anasema.

 Anasema, kila mmoja anapaswa kuwa huru kwa mwenzake, japo huwa kuna changamoto zinazoweza kusababisha mifarakano.

“Ndoa ni furaha, purukushani za kufuatana ni mambo ya kitoto, wanandoa wanapaswa kuaminiana, kuheshimiana na kila mmoja kujua mwenzake anampenda na kumlinda, kwa kufanya hivyo mtaishi vema,” anasema Mchungaji Sendoro, ambaye pia ni mwanasaikolojia.

 Kadhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Ramadhan Kitogo anasema kuna uhalali wa wenza kuchunguzana, akisisitiza kwamba ni jambo ambalo si baya, japo linapaswa kufanyika kwa busara.

 “Kuna baadhi ya watu huwa wanasema kwa maoni yao,  simu ya mume au mke hupaswi kuikagua kwa kuwa ukifanya hivyo, utagundua mambo ya kukukera.

 “Lakini ukitoa fursa hiyo kwa imani yetu maana yake unawaruhusu watu wafanye uovu huku vichaka vyao vikiwa ni simu zao.”

 Anasema wataishi kwa kanuni inayowalinda kwamba simu yake haishikwi na mwenza wake. “Hii itawapa fursa kwamba wanaishi kwenye uhalali wa ndoa ya kidini inayotambulika na Mungu, lakini unawapa kitu cha kujificha uovu wao.”

 Kadhi huyo anasema kwa muktadha wa dini haoni maana ya wenza kutofuatiliana kwa mke au mume kutokujua pilikapilika za mwenzake.

 “Usipopata kumjua mwenzako yukoje utakuwa na utulivu gani wa nafasi yako katika kuendelea kuishi naye? Hili la kuchunguzana halina ubaya, wanandoa waende nalo tu vizuri,” anasema.

 Mwanasaikolojia Modesta Kimonga anasema kumchunguza mwenza wako katika hali ya kawaida ni kukosa imani naye na kutokuwa na mapenzi ya dhati.

 “Kwenye mapenzi, inatakiwa kila mtu am-feel mwenzake, mke ahisi kupenda kama unavyopendwa, vivyo hivyo kwa mume, hali hiyo ikikosekana ndiyo inakwenda kuleta mashaka kwenye mahusiano,” anasema.

 Anasema kisaikolojia wenza wakianza kuchunguzana na kukaguana kunaashiria mapenzi hayapo tena.

“Kama yangekuwepo kusingekuwa na hofu kwamba mwenzako anachepuka, kisaikolojia love (mapenzi) unatoa kile ambacho unapokea, yaani kuwa na hisia za kupenda kama mwenzako anavyokupenda”.

 Modesta anasema ikifikia hatua kwa wenza kuanza kukaguana, kuichunguza simu ya mwenzako, hiyo ni ishara kwamba kati yao hakuna mapenzi.

 Daktari bingwa wa uzazi na wanawake, Abdul Mkeyenge anasema kuna vitu vingi kwenye uhusiano ambavyo kama wanandoa wasipokuwa makini ni changamoto hata kwenye afya ya uzazi.

Anasema magonjwa mengi, ikiwamo ya uzazi kwa wanandoa yanatokana na mtindo wa maisha wanaoishi watu wengi hivi sasa. “Kwenye mahusiano lazima mheshimiane, mpendane na kulindana, kuna watu watasema mwanaume hatakiwi kubanwa na mkewe au mume hatakiwi kumchunguza mkewe, hizi kauli ndizo zinaruhusu mtu afanye kitu fulani pasipokuwa na mipaka,” anasema.

Anasema mambo yanapoharibika haitafutwi sababu ipo wapi, bali anayetafutwa kwa wakati huo ni ‘mchawi’ yupo wapi, akibainisha kwamba katika maisha ya duniani huwa hakuna kitu kinaitwa kuridhika, hivyo hata kwenye mahusiano hali hiyo ipo, japo wanandoa wanapaswa kupendana, kulinda afya na heshima yao. “Unaweza kuwa na mke au mume, kisha ukakutana na mtu mwingine ana pesa akakuahidi kukufanyia vitu vingi, usipokuwa makini utakwenda kuharibu hata mpangilio wako wa maisha, alivyokuahidi anaweza akakufanyia au asikufanyie, lakini ukaishi katika mateso hadi ukajuta.

“Huko ndipo unaharibu mpangilio wako wa maisha, tunaona hata magonjwa yanaongezeka sababu ya mfumo wa maisha ambao unachagizwa na tamaa za kimwili na uchumi,” anasema.

Dk Mkeyenge anasema anaamini ukiwa na mke au mume ukijua mapungufu yake utamshauri na anasema kwa upande wake anaona ni jambo jema kwa wenza kuchunguzana.

“Unapompa uhuru mkubwa bila mipaka fulani, ule uhuru anaweza kuutumia vinginevyo, mfano wapo wanaosema simu ya mwenza wako usiikague, japo simaanishi kwamba kila muda uikague, la hasha, lakini hata kwa kumfuatilia mumeo au mkeo yuko wapi, anafanya nini na yuko na kina nani kuna kitu unaongeza kwenye mahusiano.”

 Anasema, mtu anayekupenda akikaa kwa saa mbili mbali na wewe, lazima atakuwaza na kukupigia simu, akieleza hali hiyo inavyoongeza thamani kwenye mahusiano.

 “Kuna wengine mume au mke ameondoka asubuhi hadi usiku hakuna aliyempigia simu mwenzake, hii inaweza kutoa mwanya mkubwa wa mtu kuchepuka. Kuna baadhi ya vitu ukiwa unaongea na mwenzako utajua yuko huru au vinginevyo, ukiwa na ukaribu naye hata kama alitaka kuchepuka kuna vitu vitamrudisha nyuma, lakini ukimuachia sana hiyo nafasi ya ukaribu akiipata kwa mtu mwingine anaitumia.

 Anasema kuna wale wanasema hawako bize na simu za wenza wao, lakini kwa kumpa uhuru huo, wapo wengine wanaanzisha mahusiano.

 “Pengine wanapanga hadi kuoana, unakuja kushtukia bomu tayari lilishakumaliza na wenyewe walishafika mbali na hisia za mwenzako zilishahama, lakini ungekuwa na kawaida ya kumchunguza ungejua mapema,” anasema.

 Japo amesisitiza katika mahusiano kila mmoja ana njia zake, ni vema mtu kutofuatisha njia za mwingine kwa sababu yule ambaye hapendi kufuatiliwa anatafuta mbinu ya kujilinda japo anaamini madhara ni makubwa.

Related Posts