MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI AJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA MPIGA KURA

Na Mwandishi wetu- Dodoma

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza Johari tarehe 16 Oktoba 2024 amejiandikisha, kwenye Daftari la Mpiga Kura katika Kata ya Ipagala Kituo cha Mbuyuni, Ilazo Jijini Dodoma ikiwa ni hatua kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 unaotarajia kufanyika Novemba 27 Mwaka huu.

Akizungumza mara baada ya kujiandikisha kwenye kituo hicho Mwanasheria Mkuu wa Serikali alitumia fursa hiyo kuwahamasisha Watumishi wote wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kujiandikisha katika Daftari la Mpiga Kura ili kutimiza haki yao ya msingi ya Kikatiba ya kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu.

“Nachukua nafasi hii kuwahamasisha Watumishi wote wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhakikisha kwamba wanatumia haki yao vizuri ya kikatiba ya kupiga kura itakapofika tarehe 27 Novemba 2024 kwa ajili ya kuwachagua Viongozi wetu wa Serikali za Mitaa”.

Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewakumbusha Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutimiza wajibu wa kujiandikisha kwenye Daftari la Mpiga Kura ili waweze kupata haki ya kushiriki kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Katika hatua nyingine Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa wito kwa Mawakili wote nchini na Wananchi kwa ujumla kushiriki zoezi la kujiandikisha kwenye Daftari la Mpiga Kura kabla ya tarehe 20 Oktoba ili waweze kupiga kura kwa kuwachagua Viongozi wa Serikali za Mitaa katika maeneo yao wanayoishi.

“Tuhakikishe kwamba kabla au ifikapo tarehe 20 ambayo ndiyo siku ya mwisho tuwe tumekwishajiandikisha wote ili tuweze kuwachagua viongozi wetu wa Serikali za Mitaa.”

Zoezi la Uandikishaji wa Wananchi katika Daftari la Mpiga kura linaendelea nchi nzima ambapo zoezi la uandikishaji lilianza tarehe 11 na linatarajia kujamilika tarehe 20 Oktoba, 2024 ikiwa ni maandalizi ya kuelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 unaotarajia kufanyika tarehe 27 Novemba, 2024.



Related Posts