Katibu Mkuu Luhemeja amesema Kaboni sio biashara


KATIBU Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mha. Cyprian Luhemeja amesema Kaboni sio biashara bali ni Utunzaji wa Mazingira wenye motisha kwa mtu ili aendelee kuhifadhi na kutunza mazingira.
Ameyasema hayo Oktoba 16, 2024 mkoani Morogoro alipotembelea Kituo cha Kitaifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) ambapo ameeleza moja ya vitu ambavyo atahakikisha vinafanyika haraka ni katika kuwekeza kwenye kaboni.
Mha. Luhemeja amewataka wale wanaojihusisha na Kaboni kuongeza kasi katika utekelezaji wa maandiko ikiwa pamoja na kuwashawishi wengine waweze kujihusisha na utunzaji wa mazingira.
“Lengo la biashara ya kaboni ni katika kuhakikisha mazingira yanatunzwa yaani fedha inayopatikana inakusaidia kwenda kutunza eneo lingine la mazingira na kuyafanya maeneo mengi kuwa salama.”
Ameongeza ni vyema makampuni katika kuwekeza kwenye kaboni wakawa wengi ili kila mmoja aone faida yake itakayomshawishi naye kuingia katika utunzaji na uhifadhi wa mazingira ambapo baada ya miaka kadhaa nchi itakuwa salama zaidi kwenye mazingira.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kituo hicho Prof. Eliakimu Zahabu amesema NCMC itaendelea kutoa ushirikiano kwa wote wenye nia ya kutaka kujua juu ya Biashara ya Kaboni ili kuvutia wawekezaji.

Related Posts