Akiwa amesaliwa na miezi michache ofisini, Rais Joe Biden anaanza ziara zake za kuaga. Atawasili nchini Ujerumani Oktoba 18. Ziara hizi zinaanza baada ya kiongozi huyo kuahirisha ile ya awali ili kushughulikia janga la Kimbunga Milton.
Kwenye ziara hii, Biden atakuwa rais wa kwanza wa Marekani tangu George H. W. Bush kutunukiwa Tuzo ya Ubora, maarufu Federal Cross of Merit ambayo hutolewa na Shirikisho la Ujerumani.
Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier atamkabidhi Biden tuzo hiyo kama ishara ya kuheshimu “juhudi alizoonyesha Biden katika ushirikiano na urafiki wa Ujerumani na Marekani, lakini pia ushirikiano baina ya Ulaya na Marekani ambao Biden mwenyewe ameendelea kuuboresha na kuuimarisha kwa zaidi ya miongo mitano, hii ikiwa ni kulingana na Ofisi ya Rais wa Ujerumani.
Uhusiano wa Marekani na Ulaya na hasa na Ujerumani, umekuwa wa karibu na ambao Biden amekuwa akiupatia kipaumbele.
Mwisho wa urais wake utaashiria mwisho wa enzi ya Biden. Je, atakuwa rais wa mwisho anayeyapigia upatu mahusiano mazuri baina ya Ulaya na Marekani?
Profesa Michelle Egan wa Chuo Kikuu cha Washington nchini Marekani na mtaalamu wa mahusiano kati ya Marekani na Ulaya ameiambia DW kwamba anadhani hiyo ni tathmini ya haki kabisa na hasa kwa sababu Biden kwa muda mrefu amekuwa akijihusisha na masuala ya Ulaya kupitia Jumuiya ya Kujihami ya NATO, mahudhurio yake kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Usalama wa Munich na pia aliwafahamu viongozi wengi wa Ulaya hata kabla ya kuwa rais, wakati alipokuwa Seneta, akihudumu kwenye kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje.
Kipi kilichombebesha dhima kubwa ya Ushirikiano na Ulaya?
Biden alizaliwa mwaka 1942 na alikulia katika nchi iliyosaidia Ujerumani Magharibi kujijenga upya baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Baada ya kujengwa kwa Ukuta wa Berlin mwaka wa 1961. Alishuhudia pia Ujerumani Magharibi ikiwa moja ya washirika muhimu wa Marekani katika Vita Baridi.
Soma pia:Von der Leyen afanya ziara nchini Marekani
Peter Sparding wa Kituo cha Masomo ya Urais na Bunge, CSPC anasema Biden amekuwa kwenye siasa tangu 1972 na alijengwa katika ulimwengu wa sera za kigeni, kupitia wa Vita Baridi na Ujerumani ikiwa ndio kitovu cha mzozo huo.
Uzoefu wake wa sera za kigeni pia ulikuwa muhimu wakati alipokuwa makamu wa rais wa Barack Obama.
Kulingana na Egan, Obama alikuwa na ujuzi mdogo sana katika sera za kigeni. Na hiyo ndiyo sababu Biden aliteuliwa kuwa mgombea mwenza wa urais. Biden alikuwa na mtandao, maarifa, na maelezo yake yalikuwa ni mafupi na hasa kutokana na jukumu lake la Seneti.
Amesema Obama alikuwa na umaarufu sana barani Ulaya kwa sababu pia alisaidia kuyajenga upya mahusiano kati ya Ulaya na Marekani baada ya kipindi cha Rais George W. Bush.
Mahusiano baina ya Ujerumani na Marekani
Ujerumani imekuwa mshirika muhimu wa Marekani chini ya Biden. Nchi hizo mbili ni miongoni mwa waungaji mkono wakubwa wa Ukraine katika vita vyake dhidi ya Urusi na zimeendelea kusimamia haki ya Israel ya kujilinda katika mzozo wa sasa wa Mashariki ya Kati.
Soma pia:Hamas yasema Biden anaipa Israel “Tiketi” ya kuendeleza vita
Egan lakini anasema pamoja na misimamo sawa kwenye jukwaa la kimataifa, masuhuba hao wanakabiliwa na changamoto zinazofanana za nyumbani kuanzia migawanyiko ya kisiasa, udhibiti wa mipakani hadi sera za uhamiaji.
Je, ndiye Rais wa mwisho wa MArekani kubeba dhima ya ushirika huu?
Biden pia anaonekana kama rais wa mwisho aliyebeba dhima kubwa ya ushirikiano huu kwa sababu umuhimu wa Ujerumani kwenye sera za nje za Marekani unazidi kupungua kuliko hapo awali. Sparding, alidokeza kuwa katika siku zijazo, Ujerumani haitaweza kuitegemea Marekani kama mtetezi wa usalama wa Ulaya.
Alisema uhusiano wa Ujerumani na Marekani utakuwa tofauti katika siku zijazo, bila kujali ni nani atakuwa rais. Marekani hivi sasa inaimarisha uhusiano na kanda ya Bahari ya Hindi na Pasifiki na kupambana na kuongezeka kwa ushindani kutoka kwa anayemuona kama mpinzani wa jadi, China. Kwa maana hiyo, matarajio ni kwamba Ujerumani itachukua majukumu zaidi ya Ulaya.
Sikiliza pia: