Mwenye namba yake anakuja, vita yabaki kwa Simba, Azam

Unaweza kusema ndani ya Simba eneo la beki wa kati mwenye namba yake yupo njiani kutua kikosini hapo baada ya klabu hiyo kufikia dau linalotakiwa na Coastal Union kwa ajili ya kumuachia Lameck Lawi.

Lawi amekuwa akiwindwa na Simba kutokana na uwepo wa taarifa za mabeki wa kati wa timu hiyo, Henock Inonga na Che Malone Fondoh kuwa njiani kuondoka baada ya kuwepo kwa ofa mezani.

Inonga anatajwa kutakiwa na FAR Rabat ya Morocco, lakini Che Malone yeye aliwahi kunukuliwa akisema anafikiria iwapo ofa itakuja na Simba kukubaliana nayo, basi yupo tayari kuondoka Msimbazi.

Simba inamtaka zaidi Lawi ili kuimarisha eneo la ulinzi pale kati baada ya kuonekana msimu huu kuna shida kwani mpaka sasa kwenye mechi 23 za Ligi Kuu Bara imeruhusu mabao 23. Hiyo ina maana imekuwa na wastani wa kuruhusu bao karibu kila mechi.

Beki wa zamani wa timu hiyo, Boniface Pawasa, amesema mwisho wa msimu ni  lazima uamuzi mgumu ufanyike kusajili beki mwingine mwenye uwezo wa kuituliza safu ya ulinzi kwa kuwa waliopo wameshindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo.

“Ukiangalia mabeki wa kati wa Simba, Che Malone na Inonga wote hawawezi majukumu ya kuwa mtu wa mwisho kila mmoja anatamani kwenda mbele kushambulia. Hilo ni tatizo la kwanza,” alisema Pawasa.

“(Simba) wanatakiwa kuboresha eneo hilo kwanza kwa sababu timu lazima iwe na mtu wa mwisho ambaye jukumu lake kubwa ni kuiongoza safu ya ulinzi.”

Hivyo basi ni wazi kwamba Lawi akitua Simba ana nafasi kubwa ya kucheza kuliko kukaa benchi kutokana na uwezo alionao.

Lakini, wakati Simba ikifika dau inalotaka Coastal Union ili kumuachia Lawi, Azam FC nayo imeingiza miguu yote miwili kumtaka beki huyo ikiweka mzigo unaotakiwa.

Kutokana na Azam na Simba zote kufikia dau ambalo Coastal Union inalitaka ili imuachie beki huyo hivi sasa uamuzi wa wapi atakwenda msimu ujao umebaki mikononi mwa mchezaji mwenyewe.

Inaripotiwa kwamba awali timu hizo mbili pamoja na Yanga kila moja iliifuata Coastal Union na dau la Sh150 milioni zikiamini lingetosha kuwashawishi ‘Wagosi wa Kaya’ kumuachia beki huyo anayesifika kwa matumizi mazuri ya akili na hesabu sahihi pindi akabilianapo na washambuliaji wa timu pinzani,  hata hivyo uongozi wa Coastal Union unadaiwa uliwekea ngumu.

Uongozi wa Coastal ulisisitiza kuwa bila ya Sh200 milioni, beki huyo mwenye umri wa miaka 18 hataenda popote na badala yake atabaki klabuni hapo kumalizia mkataba wa miaka miwili uliosalia.

Baada ya kurudi nyuma na kujipanga upya inaonekana kwamba ni kama Yanga haipo tayari kutoa kiasi hicho, lakini Simba na Azam zimejipapasa mifuko na kukubali kulipa kile ambacho timu inayommiliki mchezaji huyo inakitaka ili zipate huduma yake msimu ujao.

Habari kutoka kwa mmoja wa viongozi wa Coastal Union zimethibitisha kuwa baada ya Azam na Simba kufikia kiasi ambacho timu hiyo inakitaka ili imuachie, uongozi ulikutana juzi na kufikia uamuzi wa kutupa mpira kwa mchezaji ili aamue wapi anataka kwenda kucheza.

“Suala ambalo lipo kwa sasa ni Lawi mwenyewe kuamua anataka kuchezea timu ipi msimu ujao baada ya kuafikiana kuhusu maslahi binafsi na kwa upande wetu uongozi wa Coastal Union kokote ambako ataamua kwenda tutampa baraka zote kwa vile anaondoka akiwa ameipatia fedha klabu ambayo imemlea.

“Utaratibu wa Coastal Union miaka yote unafahamika kwamba hapa ni sehemu ya kuandaa mchezaji bora na baada ya hapo apige hatua zaidi na kuwa msaada kwa taifa na mifano iko mingi. Kwa kipaji alichonacho, timu yoyote ambayo itampata itakuwa imelamba dume,” alifichua kiongozi huyo.

Lawi msimu uliopita alikuwa mshindi wa Tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi wa Ligi Kuu Bara na msimu huu ameonekana kuwa nguzo imara ya safu ya ulinzi ya Coastal Union kwa kuifanya kuwa miongoni mwa timu ngumu kufungika msimu huu.

Wakati msimu uliopita Coastal Union ilifungwa mabao 35 baada ya mechi 30, hadi sasa timu hiyo imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 18 tu katika mechi 24 huku msimu huu ikiwa imebakiza mechi sita kumaliza msimu. Lawi amekuwa tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Coastal Union ambapo ameanza kikosini katika mechi 18 kati ya 24 ilizocheza hadi sasa msimu huu.

Related Posts