Iringa. Katibu Mkuu wa Wazazi Taifa, Ally Hapi amesema moja ya njia ya kupambana na tatizo la ubakaji na ulawiti kwa watoto ni kuwalinda na kutorihusu watembee usiku.
Amesema baadhi ya wazazi na walezi wasiojali makuzi ya watoto kiasi cha kuwatuma maeneo tofauti usiku wakati wakijua wanawaweka katika hatari ya kufanyiwa vitendo vya ukatili muda huo.
Hivi karibuni watoto watatu, mmoja akiwa wa kiume walibakwa na kulawitiwa eneo la Mtwivila, Manispaa ya Iringa baada ya wazazi kuwatuma dukani usiku.
Akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Lulanzi, wilayani Kilolo, Hapi amesema Iringa ni kati ya mikoa yenye matukio mengi ya ukatili dhidi ya watoto huku ubakaji na ulawiti ikiwa miongoni.
“Limeibuka wimbi la ukatili dhidi ya watoto hasa ubakaji na ulawiti, lazima wazazi tuwalinde watoto wetu. Msitume watoto madukani usiku, wanaenda kubakwa huko,” amesema Hapi.
“Tusipokuwa makini tutaua ndoto za watoto wetu, sio mnawaacha watoto na kwenda kupiga ulanzi, nunua ulanzi piga nyumbani,” amesema.
Aidha, amewataka wazazi kuhakikisha hawawaozeshi watoto wao walio chini ya miaka 18 na badala yake wawaache wamalize masomo yao.
“Acheni watoto watimize ndoto zao, acheni watoto wasome wala msiwe sababu ya kuwafanya waache masomo na kwenda kuolewa,” amesema.
Kiongozi huyo ambaye ziara yake ya kwanza tangu aingie madarakani ameianza Iringa, alikowahi kuwa mkuu wa mkoa.
“Mama aliponiteua nikaijenge jumuiya na mimi nilitafakari nikagundua siwezi kuijenga jumuiya hii nikiwa ofisini. Niliingia mtandaoni nikauliza Mkoa Gani uwe wa kwanza nanyi mkanikaribisha,” amesema Hapi.
Amewataka viongozi wa jumuiya hiyo kila mmoja kutimiza wajibu wake ili kuihakikishia CCM ushindi katika chaguzi zijazo.
Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Kilolo, wameiomba Serikali kuendelea kukarabari barabara zilizoharibika kwa sababu ya mvua.
Awali, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yassin amesema zipo kazi nyingi ambazo Serikali inaendelea kufanya katika kutatua kero za wananchi.
Amesema mpaka sasa baadhi ya miradi ya ujenzi wa barabara imeisha sainiwa ikiwamo ya Iringa Mjini Kilolo, imeanza kujengwa.