WANANCHI WA MAGAMBA WARIDHIA UCHIMBAJI WA BAUXITE

Na Ashrack Miraji Michuzi blog Lushoto Tanga

Wananchi wa Kata ya Magamba, wilayani Lushoto, mkoani Tanga, wamekubaliana na kuanza kwa uchimbaji wa madini ya bauxite baada ya kupata elimu ya kina kutoka kwa wataalamu wa kampuni ya Paulsam Geo Engineering Co. Ltd. Hatua hiyo inafuatia mgogoro wa muda mrefu kuhusu mradi huo.

Mkutano ulioitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Zephania Sumaye, ulihusisha wataalamu wa mazingira kutoka kampuni hiyo, ambao walitoa ufafanuzi wa kina kuhusu athari za kimazingira na kijamii zitokanazo na mradi huo, huku wakisisitiza kuwa tathmini ya kina ya athari za kimazingira inaendelea kufanyika kwenye maeneo ya leseni za uchimbaji.

Akifafanua kuhusu uchimbaji wa bauxite Magamba Mwenyekiti wa eneo hilo Mahamudu Koti alisema Abanyambo Enterprises Ltd ndiyo kampuni pekee iliyofuata utaratibu kwa kuzingatia Sheria ya madini kwa kupata mihutasari ya kuchimba madini hayo Kitongoji Cha Magamba tokea walipofika Magamba na kukubaliana na Kijiji mwaka 2001.

Aliendelea kueleza kuwa Abanyambo kwa muda mrefu waliendelea kutekeleza maelekezo mbalimbali wanayopewa na serikali hususa ni kufanya tathimini ya athari ya mazingira licha ya changamoto kadhaa katika utekelezaji wake ikiwa ni kampuni pekee iliyofuata taratibu kama Sheria ya madini inavyoelekeza iliyopata mihutasari, kuingia makubaliano na mikataba ya kufanya uchimbaji wa bauxite Magamba tokea mwaka 2001 hadi Sasa 2024.

Alisema kuwa serikali ya Kitongoji tumeweka makubaliano kisheria kwamba Kwa ajili ya kulinda mazingira hatuhitaji kampuni nyingine katika eneo hili Ili kuthibiti uchimbaji kwenye mlima bughai na maeneo ya kuzunguka Kitongoji chetu.

Aidha kwa muda wote huu ambao Abanyambo imekuwa ikifika na wataalamu wanaofanya tathimini ya mazingira wameendelea kuwa wasikivu hivyo wanaamini wakipata kibali uchimbaji wao utaleta tija kwa vijana kuinua kipato, jamii ya wanamagamba kunufaika na kukuza mapato ya Kitongoji chao kupitia ushuru.

Baadhi ya wananchi walieleza hofu yao kuhusu uwezekano wa madhara ya kiafya, hususan magonjwa kama saratani kutokana na vumbi la uchimbaji. Hata hivyo, wataalamu wa kampuni hiyo walibainisha kuwa, kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika maeneo mengine yanayochimba bauxite, hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaothibitisha athari hizo.

Julius Shilungushela, mtaalamu wa maji kutoka Paulsam Geo Engineering, aliwahakikishia wananchi kuwa vyanzo vya maji katika eneo hilo vitabaki salama. Alifafanua kuwa uchimbaji hautafanyika karibu na chanzo chochote cha maji wala kutumia vilipuzi au kemikali, bali utahusisha kuondoa tabaka la juu la ardhi, sawa na ilivyofanyika katika ujenzi wa barabara za Lushoto.

Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Zephania Sumaye, aliwataka wananchi kuwa wazalendo na kuachana na upotoshaji unaoenezwa na baadhi ya watu wasiokuwa na ujuzi wa masuala ya madini. Alisema kuwa uchimbaji huo unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa wilaya, ikiwamo kuongeza mapato ya serikali na halmashauri, huku kata ya Magamba ikinufaika moja kwa moja na mapato hayo.

Pia, aliongeza kuwa mradi huo utatoa ajira kwa vijana wa Lushoto na fursa mbalimbali za biashara, hivyo kusaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira katika eneo hilo.

Justice Mandia, mjumbe wa serikali ya kitongoji cha Magamba, akizungumza kwa niaba ya wananchi, alisema: “Tulikuwa na hofu, lakini kwa elimu tuliyopewa, tumeridhika na tunakubali kwamba mradi huu utainua uchumi wa taifa na wilaya yetu kwa ujumla.”

Wananchi hao walimpongeza Mkuu wa Wilaya kwa kufika eneo hilo na kusikiliza changamoto zao, huku wakimuomba serikali iendelee kuwa karibu nao ili kushughulikia kero zinazowakabili.

Mkutano huo ulijikita katika kujenga uelewa juu ya umuhimu wa ushirikiano kati ya jamii na wawekezaji ili kufanikisha maendeleo ya eneo hilo.




Related Posts