Hidaya, kipindupindu, mafuriko vyatishia ukuaji wa maendeleo

Dar es Salaam. Unaweza kusema baadhi ya nchi za Afrika Mashariki zipo katikati ya majanga ya asili.

Majanga hayo yametokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya baadhi ya nchi za Afrika Mashariki ambazo  zimesababisha vifo, majeraha, upotevu wa mali, uharibifu wa miundombinu na mlipuko wa magonjwa.

Hadi sasa Tanzania, Kenya, Rwanda, Burundi na Uganda ni miongoni mwa mataifa yaliyorekodi athari mbalimbali za mvua za El-Nino, ikiwamo kushuhudia vifo na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.

Inawezekana hali hii ikasumbua uchumi wa nchi hizo na kurudisha nyuma maendeleo kutokana na kulazimika kurudia walichokifanya kwa maana ya kurudishia miundombinu ya barabara iliyoharibika, makazi ya watu na matibabu ya magonjwa ya milipuko.

Tanzania yakumbwa na mafuriko

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa takribani wiki mbili zilizopita aliliambia Bunge kuwa tangu kuanza kwa mvua hizo zaidi ya watu 150 wamepoteza maisha na zaidi ya 200 kujeruhiwa, huku kaya zaidi ya 51,000 zikiwa hazina makazi baada ya nyumba zao kuathiriwa na mvua hizo.

“Maeneo mengine yaliyoathirika ni miundombinu ya shule, zahanati, nyumba za ibada, barabara, madaraja, mifugo na mashamba yenye mazao mbalimbali,” amesema Majaliwa, bungeni jijini Dodoma.

Mbali na hasara iliyotajwa na Waziri Mkuu, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa aliliambia Bunge linaloendelea kuwa Serikali inahitaji Sh500 bilioni kurejesha mawasiliano ya barabara na madaraja yaliyoathiriwa na mvua.

“Hakuna barabara hata moja, iwe ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) au Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) ambayo haijaharibiwa na El-Nino, nchi nzima mvua zimeharibu miundombinu na ili kuirejesha tunahitaji Sh500 bilioni, fedha ambazo zingetumika kwenda kwenye miradi mipya,” alisema Bashungwa.

Burundi nayo yakumbwa na mafuriko

Kwa upande wa Burundi, hivi karibuni maji katika Ziwa Tanganyika yaliongezeka na kusababisha mafuriko katika bandari ya Bunjumbura, biashara zimevurugika katika mji huo mkuu wa  kiuchumi.

Vyombo vya habari kutoka  Burundi vilieleza namna raia wa Taifa hilo dogo kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki walivyokuwa wakihangaika kukabiliana na mafuriko, baada ya mvua kubwa kunyesha nchini humo.

Kenya ni janga na mafuriko na kipindupindu

Ukiachilia mbali Tanzania na Burundi, taifa la Kenya nalo limeathiriwa na mafuriko kutokana na mvua zinazoendelea, Rais William Ruto juzi aliutangazia umma kuwa waliofariki kutokana na janga hilo walifikia 210.

Rais Ruto alitoa taarifa hiyo wakati ambao kituo cha udhibiti wa majanga cha nchi hiyo kikiwa kimeripoti kuwa mifugo zaidi ya 4,800 na ekari za mazao zaidi 27,000 zimeharibiwa, huku biashara ndogo 264 na shule 24 zikiathirika.

Mbaya zaidi, kutoka na mafuriko hayo nchi hiyo imekumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa  kipindupindu na kwa mujibu wa mamlaka za nchi hiyo, zaidi ya watu  34 wameripotiwa kuwa na ugonjwa huo hadi jana.

Katika taarifa yake, Katibu wa Afya ya Jamii na Viwango vya Kitaaluma nchini Kenya, Mary Muthoni amesema mvua zimeharibu miundombinu ya usafi na usalama wa maji. Alieleza hali hiyo imesababisha maji machafu kuchanganyika na vyanzo vingine vya maji yanayotumiwa na wananchi, hivyo kuchagiza mlipuko wa magonjwa, kikiwemo kipindupindu.

“Uhaba wa vifaa vya usafirishaji maji, uchache wa maji safi na kusambaa kwa kasi kwa maji yasiyosafishwa ni moja ya vitu vinavyotarajia kuleta athari zaidi katika ugonjwa huo,” amesema Mary.

Kwa mujibu wa Katibu huyo, wagonjwa walioripotiwa  ni wakazi wa  kaunti ya Ziwa Tana katika Kata ya Garsen Magharibi (32) na viwili ni katika Kata ya Garsen Kati. Licha ya Kenya kuripoti wagonjwa hao wa kipindupindu, hakuna taarifa zozote za mlipuko wa ugonjwa huo katika mataifa mengine ya Afrika Mashariki.

Hata hivyo, pamoja na sababu zinazotajwa kuchochea hali hiyo nchini Kenya, kuna changamoto ya usafi duni katika vituo vya uokozi wa waathirika wa mafuriko, mathalan Ziwa Tana, kumeripotiwa uhaba wa vyoo.

Mbali na kipindupindu, taifa hilo pia limeripoti wagonjwa wa matumbo ya kuhara, katika kaunti ya Marsabit.

Katika hali ya kukabiliana na ugonjwa huo, kampeni ya elimu ya afya kwa umma imezinduliwa, ikielimisha wananchi wa Kenya juu ya kukabiliana na kipindupindu.

Mtaalamu wa Afya ya Jamii nchini humo, Dk Ojwang Lusi amesema elimu ndilo jambo muhimu linalopaswa kutolewa kwa wakazi wa nchi hiyo kwa sasa.

Elimu hiyo, amesema inapaswa kujielekeza kwenye maana ya ugonjwa huo na ulivyo hatari kwa maisha ya binadamu, kadhalika mbinu za kujikinga nao.

“Tunapaswa kutoa elimu kwa watu juu ya athari za kuzembea katika kujiepusha na kipindupindu, wanatakiwa kuzingatia taratibu kama inavyoshauriwa kitaalamu,” amesema.

Watu 50 wafariki Rwanda kwa maporomoko ya udongo na radi

Waziri wa Masuala ya Dharura wa Rwanda, Albert Murasira juzi alitangaza kuwa, athari zilizotokana na mvua kubwa, maporomoko ya udongo na radi zimesababisha vifo vya watu 50 na wengine 79 kujeruhiwa nchini humo katika miezi miwili iliyopita.

Murasira amesema kuwa, watu 12 wamefariki dunia kwa kupigwa na radi, huku wengine wakifariki kwa kuangukiwa na nyumba zao mbovu.

Mvua hizo zimesababisha uharibu wa miundombinu, ikiwemo nyumba, madaraja, majengo ya shule, mitandao ya barabara na mashamba, hata hivyo, Serikali imelazimika kuwahamisha wakazi karibu 5,000 kutoka maeneo yenye hatari kubwa hadi maeneo salama.

Wakati huohuo, Rwanda, imetangaza kwamba kutokana na mvua kubwa iliyotabiriwa katika wiki ya kwanza ya Mei, baadhi ya mito inaweza kuvunja kingo zake na kusababisha mafuriko katika jamii.

Tahadhari hiyo imetolewa na Bodi ya Rasilimali za Maji ya Rwanda (RWB), na kusisitiza kuwa, mito inayoweza kusababisha mafuriko ni pamoja na Mto Sebeya, Karambo, Nyabahanga, Kabirizi, Nyabarongo, Mwogo, Mukungwa, Rubyiro, Cyagara, pamoja na mito ya Ukanda wa Virunga.

Uganda nako mambo si shwari

Kwa upande wa Uganda mvua ambazo zimenyesha hivi karibuni zimeharibu miundombinu ya barabara na madaraja ya kuelekea maeneo muhimu, jambo ambalo linaathiri shughuli za usafirishaji na ukuaji wa uchumi kwa jumla.

Kutokana na hayo yanayoendelea katika baadhi ya mataifa ya Afrika Mashariki, huenda yakatatiza matarajio yake ya ukuaji wa uchumi yaliyokuwa yanatazamiwa kuwa asilimia 5.1 kwa mwaka 2024.

Related Posts