ULINZI WAZIDI KUIMARISHWA KATIKA VITUO VYA KUJIANDIKISHA ILALA

 Mkuu wa wilaya ya Ilala Edward Mpogolo amewahakikishia wananchi ulinzi na  usalama wakati wote wa kipindi cha uchaguzi kuanzia kujiandikisha hadi upigaji kura.

Mpogolo ameyasema hayo katika muendelezo wa ziara yake ya kuhamasisha wananchi wote na makundi mbalimbali kujitokeza kujiandikisha katika daftari la makazi kwa siku mbili zilizobaki

katika kata ya Mchikichini, Buguruni, Vingunguti, Segerea, Kinyerezi, Kimanga na Tabata. 

Akiwa katika kata hizo    Mpogolo ameeleza suala la ulinzi na usalama ni endelevu katika kipindi cha uchaguzi na baada ya uchaguzi. 

Amesema wilaya ya ilala ipo salama katika kipindi chote cha uchaguzi hivyo wananchi wajitokeze kujiandikisha  katika vituo kwa siku mbili zilizobaki na wajitokeze kupiga kura tarehe 27 mwezi ujao siku ambayo itakua ni mapumziko iliyotangazwa na Mh Rais Dokta Samia Suluhu Samia. 

Akizungumza na wananchi katika ofisi za michezo ya kubahatisha maarufu kubet kata ya vingunguti Mpogolo amewahimiza kwenda kujiandikisha na kujitokeza kupiga kura. 

Mpogolo amesema kuwa kundi la vijana lina nafasi kubwa ya kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kuwa ni wanufaika wa viongozi wanaochaguliwa hivyo wahakikishe wanachagua viongozi bora. 

Akizungumzia kuhusu mikopo ya asilimia kumi Mpogolo ameeleza uwepo wa fedha katika halmashauri ya jiji  la ilala zaidi ya shilingi bilioni 11 hivyo vijana, wanawake na walemavu waunde vikundi au mtu mmoja mmoja kukopa na kukumbuka kurudisha ili wengine wakope. 

Mkuu huyo wa wilaya ya Ilala Edward Mpogolo akiambatana na Katibu tawala wilaya ya Ilala Charangwa Suleiman wameshirikiana na shirikisho la vyama vya bodaboda na bajaji Mkoa wa Dar es salaam kufikisha ujumbe wa kujiandikisha, kugawa vipeperushi kwa wananchi na makundi mbalimbali ili wajitokeze kushiriki katika uchaguzi.

Aidha Mpogolo ametumia nafasi hiyo kuwahimiza  maafisa usafirisha kuunda vikundi na kuvisajili ili watambulike na serikali ipo tayari kuwawekea mazingira rafiki ya utendaji kazi. 

Amesema kupitia viongozi wao watawezeshwa katika ujenzi wa vituo, upataji sare za maalum ili waweze kutambulika na kufanyakazi kwa uhuru.

Muuendelezo na hamasa iliyofanywa na Mkuu wa wilaya ya Ilala Edward Mpogolo ni kuhakikisha wananchi wanashiriki vilivyo uchaguzi wa serikali za mitaa wenye kauli mbiu serikali za mitaa ni sauti ya wananchi jitokeze kupiga kura.

Related Posts