Dar es Salaam. Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Tamisemi, imegomea mapendekezo ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) ya kutaka kuanza huduma katika barabara ya Mbagala (Kilwa) ifikapo Februari, 2025 ikisema ni mbali na badala yake wahakikishe huduma zinaanza mwaka huu.
Sambamba na hilo pia imewaonya kutofanya majaribio tena ya mabasi hayo kipindi cha maonyesho ya Sabasaba na kama itaamua kufanya hivyo, basi iyaache moja kwa moja.
Hayo yamejiri leo Jumamosi Mei 4, 2024 wakati kamati hiyo ilipofanya ziara ya kujionea maendeleo ya ujenzi wa miundombinu yatakapopita mabasi hayo katika mradi wa awamu ya pili inayohusisha Barabara ya Mbagala na ule wa awamu ya tatu unaohusisha Barabara ya Nyerere(Gongolamboto).
Baada ya kufika katika Barabara ya Mbagala wabunge hao walipata maelezo kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa wakala huo, Dk Athumani Kihamia, ambaye aliwaeleza kuwa tayari ujenzi wake umefikia asilimia 98.9 na matarajio yao ni huduma kuanza kutolewa rasmi Februari mwakani, baada ya kupatikana kwa mzabuni atakayeleta mabasi kwa ajili ya njia hiyo.
Kihamia amesema taratibu za kumpata mtoa huduma zinaendelea na pindi atakapopatikana inabidi apewe miezi sita kwa ajili ya kuagiza kutengenezewa mabasi hayo nje ya nchi.
“Kwa namna miundombinu ya kupita mabasi hayo ilivyotengenezwa, ni lazima utoe oda maalumu ya kutengenezewa kazi ambayo ataifanya mtoa huduma itakayochukua sio chini ya miezi sita na ndio maana tunasema itaanza kutoa huduma mwakani,” amesema.
Maelezo hayo yalionekana kutowaridhisha wajumbe wa kamati hiyo na katika majumuisho ya ziara wengi walionekana kupinga hatua hiyo, akiwamo mbunge wa viti maalumu, Hawa Mwaifunga.
“Hili la mwendokasi kuanza kazi Mbagala mwakani halikubaliki, haingii akilini kutuambia itachukua miezi sita kutengenezwa mabasi wakati duniani kote mabasi hayo yapo ni kiasi cha kuyaagiza.”
Pia, kama ninyi barabara zenu mmetengeneza tofauti na mabasi yanayopatikana huko sokoni, wekeni hata ngazi kwa muda wananchi waweze kuyatumia kuliko hiki mnachotaka kufanya sasa hivi cha kutaka yaanze kazi mwakani,” amesema Hawa.
Mbunge wa Mpanda, Sebastian Kapufi amesema kuna athari kubwa kumalizika kwa miradi mikubwa ya namna hiyo halafu inashindwa kuanza kufanya kazi kwa wakati.
“Katika hili Dart ikajitafakari kwa kuwa hata huyo kiongozi anayetafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo, huenda ikamkatisha tamaa,” amesema Kapufi.
Mbunge wa viti maalumu Salome Makamba, amesema wananchi wameshachoshwa na ahadi hizo kwa kuwa hii sio mara ya kwanza kuahidiwa huduma hiyo kuanza.
“Imefika mahali ndugu mwenyekiti huku kwenye hii miundombinu ya mwendokasi tunakuja kama kutalii, kwa kuwa ahadi hizi zilishatolewa mwaka mmoja ulioisha lakini hakuna utekelezaji.”
“Wananchi wanachotaka ni usafiri na sio maneno kila siku, isitoshe ndugu zetu wanatumia haya magari, kwa hiyo tunajua adha wanayoipata huku, tunachotaka kuona ni mabasi hayo yakianza kutoa huduma hata miezi mitatu kuanzia sasa,” amesema Salome.
Mbunge wa Temeke, Doroth Kilave amesema kitendo cha mabasi hayo kupelekwa barabara hiyo kila inapofika maonyesho ya kimataifa ya biashara, maarufu Sabasaba ifike mwisho kwa kuwa wananchi wamechoka kuhadaiwa.
“Huwa najiuliza hayo mabasi ambayo mnayaleta kipindi cha Sabasaba kwa nini msiyaache yakafanya kazi moja kwa moja katika barabara hiyo, kwani huwa mnayapeleka wapi baada ya maonyesho kuisha, safari hii naomba yasiletwe kama hamtayaacha yaendelee kuwahudumia wananchi,” amehoji Kilave.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Justine Nyamoga, amehitimisha kwa kusema kuna haja ya miundombinu ya mabasi hayo kwa awamu nyingine kujengwa kulingana na mazingira ya nchi, ili kuepuka ucheleweshaji wa kuanza kazi kwa mradi.
Pia, Nyamoga ameshauri katika miradi ya awamu zinazokuja, ujenzi wake uende sambamba na kutafuta mtoa huduma ili ujenzi tu unapokamilika na huduma zinaanza kutolewa bila kuchelewa kama ilivyo sasa.
“Kwenye ujenzi wa miundombinu niseme mpo vizuri, lakini katika utoaji wa huduma bado nachelea kuwapongeza, hivyo Dart kuna haja ya kubadilika hapa yasijirudie yaliyotokea katika awamu ya kwanza, inawafanya wananchi kuona mradi huo hauna maana kwao kutokana na uhaba wa mabasi,” amesema Mwenyekiti huyo.
Baadhi ya wananchi wa Mbagala, wakizungumzia hilo akiwamo Seleman Kaisi, amesema wanaomba Serikali iwaharakishie kufungua mradi huo kwa kuwa utawapunguzia machungu ya maisha, kwani kwa sasa usafiri wa kwenda Kariakoo wanatumia sio chini ya Sh3,000 kwa sababu ni wa shida.
Wesa Abdallah amesema watumiaji wa barabara hiyo ya Mbagala ni wengi hali inayochangia usafiri kuwa tabu na kukaa muda mrefu barabarani, hivyo kuanza kwa huduma ya mwendokasi kutawaondolea adha hiyo wakiwamo wanafunzi kuwahi shule na kuepuka kunyanyaswa na makondakta wa daladala.
Mradi wa mabasi hayo ya haraka ulianza kutoa huduma rasmi Mei 2016 na katika awamu ya kwanza mabasi yaliyohitajika ilikuwa 320 lakini yaliyokuja yalikuwa 120 na mpaka sasa mabasi yanayoelezwa kuwemo barabarani hayazidi 90.
Hali hii imekuwa ikileta adha kwa watumiaji ambako kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamika kukaa muda mrefu kwenye vituo kuyasubiri, hivyo kuchelewa katika shughuli zao za kujitafutia riziki.
Barabara ya Mbagala ikianza kufanya kazi, mabasi 750 yanatarajiwa kutoa huduma huku watu 600,000 hadi 700,000 watakuwa wakisafirishwa kwa siku.