Mkoa wa Kagera wajipanga kuingiza mabilioni kupitia ndizi

Renatha Kipaka, Kagara

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatuma Mwasa amesema wamejipanga kuingiza kiasi cha sh 96 bilioni kupitia programu ya kilimo ya miaka mitatu kutokana na mpango wa kupanua ekari 10, 000 ili kuinua uchumi wa mkoa huo.

Amesema hayo wakati kilele cha maadhimisho ya siku ya chakula duniani ambapo kwa mwaka huu yamefanyika mkoani Kagera.

Amesema uwepo wa programu ni mkakati wa kuinua uchumi wa Kagera kupitia kilimo kwa mazao yanayolimwa na kustawi.

Amesema sambamba na program hiyo mkoa unatoa ombi maaalumu kwa wizara ya kilimo la kujenga masoko kwa zao la ndizi katika mipaka ili kumwezesha mkulima kuinua uchumi .

Mwassa amesema mkoa una mchango mkubwa katika uzalishaji wa mazao mbalimbali ya biashara na chakula ambapo ni ndizi, mkulima anapata manufaa kidogo ikilinganisha na wakulima wa mazao mengine.

Hata hivyo amesema kuwa masoko ya mipakani yatawasaidia wakulima kupanua wigo na masoko ya nje ikiwemo kuwafikia wafanyabiashara wanaoshusha thamani ya zao kwa kufuata mkulima shambani.

“Mkungu mmoja wa ndizi kilogramu 50 unauzwa kutoka kwa mkulima wa Karagwe,Kyerwa na Muleba ni shilingi 3000 hadi 10,000 hii sio sawa ,kwenye mikoa mingine wanauza hadi sh 40,000, tuna wafanyabiashara wengi wanaotoka katika mataifa jirani kuja kununua ndizi lakini hawawezi, kutoka kwa mkulima. Tunaamini kupitia mipaka yetu mingi kama tutakuwa na soko la ndizi la kudumu wakulima watanufaika na bei ya zao hilo,”amebainisha Mwassa.

Ameeleza kuwa kutokana na uzalishaji wa zao la ndizi kuwepo kwa wingi mkoa wa Kagera usingeonekana kuwa chini kiuchumi na kungekuwa na uimarishaji wa masoko ndizi zinazovushwa kwenda nje zingemsadia mkulima.

Naye Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amesema kuwa swala la ujenzi wa soko la ndizi katika Wilaya zinazozalisha ndizi kwa wingi kama Mkoa wa Kagera serikali italifanyia kazi kwa vitendo kwa kujenga soko la kisasa.

Aidha amesema kuwa kwa sasa Taifa limezalisha chakula kwa asilimia 128 na ongezeko la chakula kila mwaka kwa mwaka wa fedha 2023/2024 uzalishaji ulikuwa tani miloni 22.8 mahitaji ni milioni 17.7 na kuwa na zaidi ya chakula tani 5.05.

Amesema kuwa serikali inahakikisha kwamba inafanya mabadiliko ya kilimo cha mazoea ambacho kitamsaidia mkulima katika kuwa na mategeo ya umwangiliaji na sio mvua.

Hata hivyo amesema bajeti ya tume ya umwangiliaji imepandishwa kutoka kiasi cha Sh.bilioni 22 hadi kufikia 408 katika mwaka wa fedha 2024/2025 ambayo inaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo na sio matumizi ya kawaida.

Kwa upande wake Juma Kahabuka ambae ni mkulima wa ndizi na mkazi wa Kyerwa amesema kuwa kilimo hicho kimekuwa msaada mkubwa kwenye familia yake kwani amekuwa akisomesha watoto wake kupitia zao hilo.

Kahabuka amesema kwa mwaka huu katika shamba lake kwa kipindi cha Agosti h alikuwa anauza mikungu 15 kwa siku ambayo ilikuwa ikiuzwa kwa shilingi 5000 kila mmoja.

Related Posts