THRDC wataka taasisi zinazohusika na uchaguzi kujikumbusha sheria, kanuni

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umezitaka taasisi zinazohusika na uchaguzi kuona umuhimu wa kujikumbusha sheria na kanuni za uchaguzi ili kuhakikisha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu unaendeshwa kwa amani na utulivu.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unatarajiwa kufanyika Novemba 27,2024 wakati Uchaguzi Mkuu unatarajiwa kufanyika mwaka 2025.

Akizungumza Oktoba 18,2024 wakati wa kufungwa mafunzo yaliyowahusisha makamanda wa polisi wa mikoa na wasaidizi wao Mratibu Kitaifa wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, amesema baadhi ya changamoto zinazojitokeza wakati wa uchaguzi zinasababishwa na makundi mengine.

“Tunataka kuona michakato ya demokrasia inaendeshwa kwa misingi ya kikatiba, sheria na haki za binadamu. Hatupendi kukemea ukiukwaji wa haki za binadamu bali kuzuia usijitokeze,” amesema Olengurumwa.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa, amesema wamekumbushwa mambo ya msingi yanayohusu uchaguzi kwa sababu jeshi hilo lina kazi kubwa ya kulinda haki za binadamu wakati wote wa uchaguzi.

“Mafunzo yamekuwa muhimu kwetu kwa sababu tunakwenda katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mwaka 2025 tunaingia katika Uchaguzi Mkuu, yatatuimarisha katika kusimamia uchaguzi kwa kufanya kazi kwa bidii na kuweka mbele haki za binadamu,” amesema Mutafungwa.

Akifunga mafunzo hayo Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhan Kingai, amesema ni muhimu jeshi liwe na weledi wa kutosha katika kudumisha haki za msingi za raia wote hivyo mafunzo hayo yataongeza maarifa kwa watendaji wake.

“Maarifa mliyoyapata muyafikishe katika himaya zenu ili kila mmoja akatende haki kwa mujibu wa sheria kwa kuzingatia haki za binadamu…wananchi wakituamini watatupa ushirikiano mkubwa na uchaguzi utakuwa salama,” amesema Kingai.

Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyokuwa na mada sita washiriki walikumbushwa mambo ya msingi yanayoendana na majukumu yao hasa wakati wa uchaguzi zikiwemo sheria mbalimbali zinazosimamia uchaguzi, miongozo ya kimataifa inayosimamia usalama na viashiria vya uvunjifu wa haki za binadamu wakati wa uchaguzi.

THRDC inaamini mafunzo hayo yana faida kubwa kwa nchi kwa kuwa jeshi la polisi litarudisha imani kwa wananchi na kuweza kukabiliana na mazingira yoyote ya kuvuruga amani wakati wa uchaguzi.

Related Posts