Mohamed Abu Jalda ambaye kwa sasa anaishi katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao baada ya kutoroka nyumbani kwake, anafanya mazoezi kwenye ufuo wa bahari katika eneo la Al-Mawasi huko Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Alizungumza na Ziad Taleb wa UN News.
“Mimi ni Mohamed Abu Jalda, mchezaji wa Klabu ya Rafah Services, timu ya soka ya daraja la kwanza huko Gaza.
Nilikuwa na nia kubwa ya kuwa mchezaji bora wa kandanda kama wengine nje ya Ukanda wa Gaza, lakini kwa sababu ya vita, matarajio yangu na maisha yangu yalichelewa. Sasa nina umri wa miaka 20, nikijaribu kuwa mtaalamu, lakini siwezi kwa sababu ninaishi Gaza chini ya moto wa mara kwa mara.
Kila siku ninahisi kama ninakufa; Mungu atupe subira ya kustahimili maisha haya. Ninatoka Rafah, lakini sasa ninaishi katika kambi ya Shaboura ya watu waliohamishwa katika eneo la Al-Mawasi huko Rafah.
Ni miezi mitano imepita tangu nihamishiwe huko.
Wakati wowote ninapopata muda wa kupumzika na kujisikia kucheza kandanda, mimi huelekea ufukweni, mahali pekee ambapo ninaweza kucheza.
Tulihamishwa na hakuna mtu aliyekuja kututafuta. Nataka sauti yangu ifikie ulimwengu.
Ndoto yangu na matamanio yangu ni kucheza mpira wa miguu. Nimekuwa na tamaa hii tangu nikiwa na umri wa miaka 10, lakini sasa nina zaidi ya miaka 20, na sioni chochote kwa sababu ninaishi Gaza chini ya ukandamizaji huu.
'Ni nini kinachonifanya kuwa tofauti?'
Kwa nini siwezi kuwa mchezaji wa mpira wa miguu? Ni nini kinachonifanya kuwa tofauti na mtu mwingine yeyote duniani? Nina masikio kama yao, pua kama yao, na miguu kama yao; hakuna tofauti.
Kwa sababu ya vita, hakuna fursa zilizonijia. Kabla ya vita, nilikuwa sawa kimwili, lakini sasa mambo yamebadilika kutokana na kuhama tunakoishi.
Ninajaribu kufanya mazoezi kila baada ya siku tatu ufukweni ili kutimiza azma yangu na ninatumai kwamba sauti yangu itafikia ulimwengu, kwa sababu nina haki ya kuwa mwanasoka wa kulipwa kama mtu mwingine yeyote.
Natumaini kwamba Mungu atanijaalia mafanikio ya kuwa mchezaji wa soka.
Ninajivunia kuwa kutoka Gaza na ninatumai kuchezea timu ya taifa ya Palestina, kwa sababu hii ni haki yangu.
Waache wanijaribu, na nitaonyesha ujuzi wote nilionao katika soka.”