WATUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUWALINDA WATOA TAARIFA JUU YA VITENDO VYA UKIUKWAJI WA MAADILI

Na Mwandishi wetu Dodoma

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi,amewataka watumishi wa umma nchini kuimarisha mifumo madhubuti na taratibu za kuwalinda watoa taarifa juu ya vitendo vya ukiukwaji wa maadili na rushwa mahali pa kazi.

Mkomi ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akifunga kikao cha kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na utawala bora baina ya taasisi zinazohusika na usimamizi wa maadili na mamlaka za kitaaluma.

Mkomi amesema kuwa umuhimu wa kuimarisha mifumo ya ulinzi kwa watoa taarifa juu ya vitendo vya ukiukwaji wa maadili. Amesema mifumo madhubuti ya kuwalinda watoa taarifa inapaswa kuwepo ili kuzuia watu wanaotoa taarifa kudhurika.

Amebainisha kuwa hatua zitachukuliwa dhidi ya watumishi wanaothibitika kukiuka maadili, hususan wanapojihusisha na vitendo vya rushwa, akisisitiza kwamba rushwa ni kosa la jinai na sheria itachukua mkondo wake.

“Kumekuwa na vitendo vingi vya ukiukwaji wa maadili ya utumishi wa umma vinavyofanywa na watumishi wa umma, hivyo lazima hatia zichukuliwe dhidi ya wanaokiuka,”amesema Mkomi

Hata hivyo ameeleza kuwa ili tuweze kupunguza vitendo vya rushwa mahali pa kazi ni lazima tuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma kwa watumishi wa umma serikalini.

“Ili tufanikiwe kutatua changamoto za maadili lazima tutumie TEHAMA. Ni wazi kuwa matumizi ya TEHAMA yataondoa ulazima wa mikutano ya ana kwa ana kati ya mtoa huduma na muhitaji, hali itakayopunguza vitendo vya rushwa mahala pa kazi,” amesema Mkomi

Mkomi amesema kuwa matumizi ya TEHAMA ni muhimu katika kuboresha maadili na kupunguza mianya ya rushwa na kuweka utawala bora katika sekta ya utumishi wa umma nchini.

Aidha amesema kuwa watumishi wa umma nchini wanapaswa kupewa mafunzo ya masuala ya maadili mara wanapoingia kazini, huku akisisitiza umuhimu wa kanuni za maadili ya utendaji kuwekwa wazi na kupatikana kwenye tovuti rasmi za ofisi husika.

Pia Mkomi amesisitiza umuhimu wa kufanya tathmini ya kina kuhusu utendaji wa watumishi, ikijumuisha tabia na mienendo yao wakati wote.

“Tabia na mienendo ya watumishi lazima ifanyiwe tathmini, hatua hii itasaidia kuhakikisha kuwa wale wanaopandishwa vyeo ni wale walio na maadili mema na si kwa sababu tu wamefanya kazi kwa miaka mingi,” amesisitiza.

Awali Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Maadili katika Utumishi wa Umma, Leila Mavika, amesema kuwa kikao hicho kilikuwa na lengo la kuimarisha maadili ya utumishi wa umma.

“Tumepitisha maazimio matano yakilenga masuala ya maadili na taaluma,” tutahakikisha tunayafanyia kazi kama.viongozi wakuu walivyoelekeza amesema Mavika.

Kikao hicho cha siku mbili kililenga kuboresha mifumo ya utawala bora na kuondoa mianya ya rushwa katika sekta ya umma, huku TEHAMA ikionekana kama nyenzo muhimu katika kufanikisha malengo hayo





Related Posts