Afrika kujadili haki ya Umiliki wa Ardhi kwa vijana

Na Seif Mangwangi, Arusha

Migogoro ya kisiasa katika nchi nyingi za kiafrika na kutokuwepo kwa sera za kuwezesha vijana kumiliki ardhi ni miongoni mwa changamoto zinazoelezwa kuchangia umaskini kwa vijana barani Afrika.

Hayo yameelezwa leo Oktoba 20,2024 Jijini hapa na waandaaji wa Kongamano la Kimataifa kuhusu vijana na utawala wa Ardhi barani Afrika (CIGOFA4), linaloanza kesho Jijini hapa katika kikao chao na Waandishi wa habari.

Mkurugenzi wa taasisi ya Youth Initiative for land in Afrika(Yilaa), Augustine Nyakatoma amesema lengo kuu la kongamano hilo ni kusaidia vijana kupata haki na uelewa katika kumiliki ardhi sanjari na kusaidia kutoa uelewa kwa viongozi ili waweze kusaidia vijana kumiliki ardhi.

Amesema ardhi ni Uhai hivyo ni muhimu kuhakikisha vijana wanamiliki ardhi na kuitumia kujipatia kipato hususani katika nyakati hizi ambazo ukosefu wa ajira umekuwa ni tatizo kubwa.

” Vijana wanategemea kurithi ardhi kutoka kwa wazazi wao lakini hakuna utaratibu wa kuwezesha wamiliki ardhi hiyo,”amesema Augustine.

Aidha amesema Tanzania imekuwa ikijitahidi kusaidia vijana kumiliki ardhi lakini hakuna utaratibu wa kisera kuwezesha kijana kumiliki ardhi husika.

Zaidi ya vijana 500 kutoka pande zote za bara hilo watashiriki katika mkutano huo wa nne utakaofanyika pia kwa njia ya Mtandao(Zoom).

Mratibu wa nchi zinazozungumza Kiingereza katika Jumuiya hiyo, Deborah Oyugi amesema pia mkutano huo utajadili nafasi ya mwanamke na mtoto wa kike katika umiliki wa Ardhi barani Afrika.

” Kutokana na maazimio yaliyotolewa katika mikutano mingine mitatu ya CIGOFA, tutajadil nafasi ya mwanamke na mtoto wa kike katika masuala ya umiliki wa Ardhi.

” Sasa hivi kundi hilo wanashirikishwa kwa kiasi fulani katika masuala ya Ardhi, lakini tunataka washirikishwe zaidi hadi katika ngazi ya maamuzi,” anasema Mratibu huyo.

“CIGOFA 4 inalenga kuwawezesha vijana kwa kutoa jukwaa la mazungumzo,kubadilishana maarifa,na ushirikiano katika masuala muhimu yanayohusiana na haki za Ardhi kwa vijana

“Pia watajadili mabadiliko ya tabia nchi na vijana,na maendeleo endelevu,” amesisitiza Ofisa Mtendaji huyo Mkuu.

Mkutano huo utawahusisha washiriki kutoka sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wawakilishi wa serikali,mashirika ya kiraia,vijana,washirika wa maendeleo, wasomi na viongozi wa vijana.

Mratibu wa Jukwaa la Ardhi Tanzania, Bernard Baha amesema pamoja na jitihada mbalimbali za kuwashirikisha vijana katika masuala ya Ardhi,bado elimu zaidi inahitajika ili waelewe haki katika umiliki wa Ardhi.

Mkutano huo umeandaliwa kwa pamoja na YILAA kwa kushirikiana na Umoja wa Afrika(AU),Shirika la Maendeleo la Ujerumani(GIZ) na Muungano wa Kimataifa wa Ardhi (ILC).

Washirika wengine waliofanikisha mkutano huo ni Mtandao wa Vijana wafanyao upimaji(FIG), LANDESA,Muungano wa Ardhi wa Tanzania na wadau wengine.

Related Posts