WAZIRI MCHENGERWA AFUNGA ZOEZI LA UANDIKISHAJI DAFTARI LA MPIGA MPIGA KURA

 

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala  za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI ) Mohammed  Mchengerwa leo 20,Oktoba 2024  amefunga zoezi la kujiandikisha kupiga kura na kutoa taarifa ya siku tisa ya waliojitokeza kujiandikisha nchini ambapo watanzania zaidi ya Mil. 26,769,995 wamejiandikisha sawa na asilimia 81.15  ya Watanzania wamejiandikisha.

Mhe. Mchengerwa amejiandikisha katika Kituo cha uandikishaji cha Umwe Mchikichini  kilichopo Jimboni kwake Ikwiriri Wilaya  ya Rufiji Mkoa wa Pwani ambapo ametumia nafasi hiyo kuzungumza  na wananchi  na Waandishi wa Habari Jimboni kwake mara baada ya kujiandikisha  kwenye daftari la mpiga kura na kusema kuwa zoezi hilo litafungwa ifikapo saa12 jioni leo.

Mhe.Mchengerwa  amesema kuwa  taarifa ya  jumla  itatolewa ifikapo saa sita usiku leo  na kusisitiza kuwa muda hautaongezwa.

“Nawapongeza wananchi kwa kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari  la mpigakura  kote nchini ambapo waliojiandikisha  kwa mujibu wa taarifa ya awali ni asilimia hizo 81. 15” amesema.

Aidha Mhe.Mchengerwa  ameitaja Mikoa iliyoongoza kwenye zoezi la kujitokeza kujiandikisha  kuwa ni Tanga uliopata asilimia  101.13 Mkoa wa Pwani  asilimia    98.78,huku Mwanza  94.09 ukifuatiwa na Mkoa wa  Dar 86.66 5 Dodoma 80.63

“Mtakumbuka kuwa kwa muda wa siku 9 sasa toka tarehe 11 Oktoba, 2024 Wasimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wamekuwa katika zoezi la kuandikisha Watanzania watakaoshiriki zoezi la upigaji kura kuchagua viongozi wa Serikali za Mitaa itakapofika tarehe 27 Novemba, 2024. Uandikishaji huu unafanyika kwa muda wa siku 10 hadi tarehe 20 Oktoba, 2024” amesema Mchengerwa.

Amesema kuwa uandikishaji na maandalizi ya orodha ya wapiga kura wa Uchaguzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ni takwa mojawapo la kanuni za Uchaguzi wa namlaka za Serikali za Mitaa za mwaka 2024.

“Kanuni hizo zinaelekeza kuwa kutakuwa na orodha ya wapiga kura ambayo itatumika katika uchaguzi wa kuwachagua mwenyekiti wa Kijiji, mwenyekiti wa mtaa, Mwenyekiti wa Kitongoji na Wajumbe wa Serikali za Vijiji na kamati za mitaa” amesema.

“Nimeona nikutane nanyi ili kuwafahamisha Watanzania kuhusu mwenendo wa uandikishaji huo hadi kufikia siku ya 9  tarehe 19 Oktoba, 2024 na kutoa wito kwa Watanzania ambao hawajajitokeza kujiandikisha watumie siku ya leo ambayo pia ni siku ya mapumziko” amesema.

“Jumla ya wapiga kura 26,769,995 wamejiandikisha kupiga kura sawa na asilimia 81.15 ya lengo la kuandikisha watu 32,987,579 kwa siku zote 10 ambapo wanaume ni 13,033,988 sawa na asilimia 48.69 ya watu wote waliojiandikisha kwa tarehe 11-19 Oktoba, 2024 na wanawake ni 13,736,007 sawa na asilimia 51.31 ya watu wote waliojiandikisha”

“Kwa ujumla, mwenendo huu ni mzuri sana, na kama utaendelea hivi kwa siku ya leo, uwezekano wa kufikia malengo ya uandikishaji ni mkubwa. Hii ni kwa kuwa kuanzia siku ya 5 hadi ya 9 kumekuwa na kuongezeka kwa idadi ya Watanzania waliojitokeza kujiandikisha

Siku ya 5 tarehe 16 Oktoba, 2024 waliandikishwa jumla ya wapiga kura 2,460,664 sawa na asilimia 7.46 ya lengo la siku” alisema.

“Siku ya 6 tarehe 16 Oktoba, 2024 waliandikishwa jumla ya wapiga kura 2,472,605 sawa na asilimia 7.50 ya lengo la siku; siku ya 7 tarehe 17 Oktoba, 2024 waliandikishwa jumla ya wapiga kura 2,971,219 sawa na asilimia 9.01 ya lengo la siku Siku ya 8 tarehe 18 Oktoba, 2024 waliandikishwa jumla ya wapiga kura 3,409,211 sawa na asilimia 10.33 ya lengo la siku; siku ya 9 tarehe 19 Oktoba 2024 waliandikishwa jumla ya wapiga kura  3,813,999 sawa na asilimia 115.6 ya lengo la siku”

“Mikoa mitano yenye asilimia kubwa ya uandikishaji hadi kufikia tarehe 18 Oktoba, 2024 ambayo ni siku ya 8 ya uandikishaji ni Tanga umefikia asilimia 101.13%  ya malengo; Pwani umefikia asilimia  98.74% ya malengo; Mwanza umefikia asilimia  94.09% ya malengo

Dar Es Salaam  umefikia asilimia  86.66% ya malengo; na Dodoma umefikia asilimia 80.63% ya malengo”

Amesema sababu za Mikoa hiyo kuongoza ni pamoja na kukaribia kufikia malengo ya uandikishaji, Mikoa hii pia ni miongoni mwa Mikoa yenye idadi kubwa ya watu wenye umri wa kupiga kura. 

Aidha Mheshimiwa Mchengerwa alimshukuru Watanzania kufuatia mwenendo huu mzuri wa uandikishaji, nichukue fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza Watanzania wote waliojitokeza kujiandikisha hadi kufikia tarehe 19 Oktoba 2024 kwa kuwa tayari wamejiwekea mazingira kubalika ya kisheria ya kutekeleza haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wa Serikali za Mitaa wanaowataka ifikapo tarehe 27 Oktoba 2024 siku ya kupiga kura.

Hata hivyo, ametoa wito kwa Watanzania wenye sifa ambao bado hawajajitokeza kujiandikisha, kutumia siku ya leo ambayo ndiyo ya mwisho kujitokeza kujiandikisha ili kutimiza haki yao ya kikatiba ya kuwachagua viongozi wanaowataka. Kwa kufanya hivyo, pia watakuwa wamemuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye tayari amejiandikisha toka siku ya kwanza ya uandikishaji, tarehe 11 Oktoba, 2024 na amekuwa akihimiza kila mmoja wetu kutimiza jukumu hilo la kikatiba.

“Aidha, naomba nitumie fursa hii kuendelea kuwaomba wadau mbalimbali wakiwemo vyombo vya habari, viongozi wa dini, viongozi wa kimila, asasi za kiraia na wadau wengine kuendelea kuwahamasisha na kuwaelimisha watanzania wenye sifa wajitokeze kwa wingi katika siku ya leo ili kujiandikisha”. 

“Pia nitoe rai kwa Wananchi wenye sifa za kuchaguliwa kuwa Viongozi wajitokeze kuanzia tarehe 26 Oktoba hadi tarehe 1 Novemba, 2024 ili waweze kutimiza haki yao ya kikatiba kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi huu. Zoezi la kuchukua na kurudisha fomu litafanyika kwa siku hizo zote.  Muda wa kampeni utakapofika zifanyike kampeni za kistaarabu na kudumisha hali ya utulivu na amani” 

“Niendelee kuwashukuru wananchi wote, wanachama na wapenzi wa vyama vyote vya siasa kwa kuendelea kuonesha ukomavu wa kisiasa kwa kufanya siasa za kistaarabu, siasa za hoja na si za ugomvi mpaka sasa, niwasihi tuendelee  hivyo na nikemee vikali wale wachache waliotaka kuleta siasa za ugomvi na kuhatarisha amani ambazo hakika hatutaziruhusu katika uchaguzi huu”

“Nivisihi na kuviomba vyombo vya dola viendelee kuhakikisha kuna amani na utulivu tunapoendelea na mchakato huu ili Wananchi wote waweze kushiriki zoezi hili kwa amani na Utulivu”

“Wasimamizi wa Uchaguzi na wadau wote wa uchaguzi kuendelea kuzingatia Sheria na Kanuni za Uchaguzi ili kuhakikisha kuwa uchaguzi huu unaendelea kuendeshwa kwa misingi ya Sheria na Kanuni zilizowekwa” amesema.

Related Posts