Mdhibiti ubora elimu aitaka St Anne Marie Academy ifundishe kichina

 

 Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imeipongeza shule ya St Anne Marie Academy kwa kuanza kufundisha lugha ya kifaransa na kuishauri kuanzia mwakani ianze kufundisha lugha ya kichina kwani soko lake ni kubwa duniani.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mdhibiti Ubora Mkuu wa Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam, Elikana Manyilizu, wakati wa mahafali ya 23 ya shule ya awali iliyofanyika shuleni Kimara Mbezi kwa Msuguri.

Alisema kwa ulimwengu wa sasa watu wanapaswa kuchangamkia lugha za kigeni kwani zinawawezesha wanaozijua kupata kazi kwa urahisi .

Manyilizu alishauri uongozi wa shule hizo kuanza kufundisha lugha ya kichina kuanzia mwakani kwani lugha hiyo imekuwa na soko kubwa duniani kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na wawekezaji raia wa China.

“Nawapongeza sana kwa kuanza kufundisha kifaransa kwasababu mnatekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyeagiza lugha hii ifundishweni shuleni na pia nawashauri mwakani muanze kufundisha pia lugha ya kichina,” alisema

“Katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia lugha ambayo mahitaji yake ni makubwa sana na yanazidi kuongezeka ni lugha ya kichina na kama hamna walimu mimi nina rafiki yangu pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam njooni nitawasaidia kupata walimu,” alisema

Alimpongeza Mkurugenzi wa shule hiyo, Dk. Jasson Rweikiza kwa uwekezaji mkubwa alioufanya hali ambayo alisema inaisaidia serikali kuwafikia watanzania wengi kupata elimu.

“Hata matokeo ya kidato cha nne mwaka huu shule hii imepata daraja la kwanza, lapilli na daraja la tatu tu hakuna daraja la nne wala sifuri haya ni matokeo mazuri sana na wazazi lazima mjivunie kwamba mmewekeza kwenye shule sahihi,” alisema

Mkurugenzi wa shule hiyo, Dk. Rweikiza alisema mtoto ambaye mzazi wake anayemlipia ada atafariki ataendelea na masomo bila kulipa ada mpaka atakapomaliza shule na kwamba hakuna mwanafunzi atakayefukuzwa.

“Wakati wa mlipuko wa UVIKO shule zetu zilipoteza wazazi 42, watoto walihangaika sana tukakaa na bodi ya shule tutakukubaliana kuwa mzazi anayelipa ada akifariki basi kama ni wa shule ya msingi aendelee mpaka atakapomaliza na kama ni wa sekondari aendelee mpaka atakapomaliza,” alisema

“Hata elimu inayotolewa hapa ni ya viwango, huwa hakuna daraja la nne wala sifuri kwenye shule yetu, mkuu wa shule ni wa viwango anakesha akihangaikia ubora wa shule hii kwa kuhakikisha walimu wanatimiza wajibu wao,” alisema

Alisema shule imeajiri wadhibiti ubora wa ndani  na ina bodi ya mitihani ambayo inatunga mitihani

“Mwalimu hapa St Anne kazi yake ni kufundisha kazi ya kutunga mitihani tumeipa bodi ya mitihani kwasababu tuliona mwalimu akifunsisha mwenyewe akatunga mitihani mwenyewe anaweza kupendelea kwenye silabasi alizofundisha tu akaacha zile ambazo hakuzikamilisha,” alisema

“Sasa bodi ikitunga mitihani kama silabasi zilikuwa tano watatunga mtihani kwenye silabasi zote na mwanafunzi akifeli mwalimu atapaswa kujieleza kwanini wanafunzi wamefeli mtihani wake,” alisema Dk. Rweikiza ambaye ni Mbunge wa Bukoba Vijijini (CCM).

Mwisho

Related Posts